Mwanza. Shule za awali na msingi zenye uhaba mkubwa wa madawati jijini Mwanza zimepokea mgawo wa madawati 2,939, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya wanafunzi kusomea chini na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Shule hizo ni pamoja na Nyasubi (madawati 238), Kishiri (350), Bulale (300), Nyangulugulu (234), Igelegele (146), Amina Makilagi (170), Nyakabungo B (191), Nyakabungo C (90), Lake (110), Sahwa (300), Bugayamba (130), Samia (350) na Nyerere (330).
Madawati hayo yamekabidhiwa leo, Ijumaa, Februari 13, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Mtanda ameziagiza pia halmashauri zenye upungufu mkubwa kujenga karakana zao ili zitengeneze madawati kwa gharama nafuu na kumaliza tatizo lililopo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akimpa fedha ya kununua viatu mwanafunzi wa Sekondari ya Kisoko baada ya kumuona na yeboyebo wakati akizindua shule hiyo, akiagiza wanafunzi kutorudishwa nyumbani kwa kukosa sare za shule. Picha na Saada Amir
Akizungumza baada ya kukabidhi madawati hayo, Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza una upungufu wa madawati 61,808, huku Jiji la Mwanza likiongoza kwa kuwa na upungufu wa madawati 16,000.
Ametaja wilaya nyingine zenye upungufu huo ni pamoja na Kwimba (10,260), Magu (7,653) na Sengerema (8,523).
“Hatutarajii kuona mwanafunzi anakaa chini wakati tuna uwezo wa kutengeneza madawati hapa hapa. Naagiza halmashauri zote zenye upungufu mkubwa kuanza mara moja kujenga workshop zao. Ndani ya miezi mitatu tutaanza kuzitembelea kuona utekelezaji,” amesema Mtanda.
Amesema kupitia mradi wa utengenezaji na usambazaji wa madawati wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, zaidi ya madawati 4,000 yamesambazwa katika shule za awali na msingi jijini humo, huku awamu ya pili ikitarajiwa kusambaza madawati 12,000 kufikia Juni 2026.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mchumi wa Jiji la Mwanza, Mariam Mzaga, amesema mahitaji ya madawati katika jiji hilo ni 36,261, yaliyopo ni 19,504, na hivyo kuwa na upungufu wa 16,757.
“Katika awamu ya kwanza, tumetengeneza madawati 2,939 kwa gharama ya Sh440.8 milioni. Awamu ya pili ya madawati 2,061 yenye thamani ya Sh309.1 milioni ipo katika hatua za mwisho kabla ya kuingia mkataba,” amesema Mzaga.
Baadhi ya wazazi wa Kata ya Luchelele jijini Mwanza wakishuhudia uzinduzi wa shule ya Sekodari Kisoko. Shule hiyo imezinduliwa Februari 12, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda. Picha na Saada Amir
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, ameahidi kumaliza upungufu wa madawati 12,000 yaliyosalia ndani ya jiji hilo kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.
“Shule ya msingi Kishiri ina wanafunzi 4,002, kwa hiyo tumeanza na hawa wenye uhitaji mkubwa, halafu tutakuja kwa hawa wadogo wadogo mpaka kufikia mwezi wa sita, madarasa yote tuliyonayo yatakuwa yamejaa madawati 30 kila darasa,” amesema Kibamba.
Katika hatua nyingine, Mtanda ameagiza wanafunzi 4,246 wa kidato cha kwanza ambao hawajaripoti shuleni kati ya wanafunzi 15,509 waliopangwa kujiunga na kidato hicho mwaka 2026 mkoani Mwanza watafutwe popote walipo.
“Walioripoti hadi sasa ni 10,746, sawa na asilimia 76… Nawaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wa kata kuwatafuta popote walipo wanafunzi hawa na kuhakikisha wanaripoti ndani ya wiki mbili,” amesema.
Amesisitiza kuwa hakuna mwanafunzi anayepaswa kurejeshwa nyumbani kwa kukosa sare, viatu au michango; badala yake, walimu wawabane wazazi ambao wana wajibu wa kuwanunulia watoto wao vifaa kwa kuweka makubaliano nao.
“Maagizo ya Waziri wa Elimu yako wazi; mwanafunzi asirudishwe nyumbani kwa sababu ya michango. Kaa na mzazi, weka makubaliano ya namna ya kulipa, lakini mtoto aendelee na masomo,” amesema.
Mbali na kukabidhi madawati, Mtanda amezindua Shule ya Msingi Kanyerere iliyojengwa kwa zaidi ya Sh424.8 milioni kupitia ushirikiano wa wananchi, wadau na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkuu wa shule hiyo, Peter James, amesema shule ilianza kujengwa Desemba 2023 kwa nguvu za wananchi walioweka misingi 10 ya madarasa kabla halmashauri haijakamilisha ujenzi kuanzia Aprili 2024.
Shule hiyo ilianza kutoa huduma ya elimu Novemba 2025, na ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja imefikisha wanafunzi 1,110’, kati ya hao, wasichana ni 583 na wavulana 527.
Amesema wanafunzi 808 walihamishwa kutoka Shule ya Msingi Tambukareli, hali iliyopunguza msongamano katika shule hiyo kutoka uwiano wa wanafunzi 250 kwa darasa hadi 100 kwa darasa.
“Ujenzi huu umeboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza umbali wa wanafunzi waliokuwa wakitembea kutoka maeneo ya Kanyerere na Kona ya Bajaji kwenda Tambukareli,” amesema James.
Shule nyingine iliyozinduliwa na mkuu huyo wa mkoa ni Sekondari ya Kisoko iliyopo Kata ya Luchelele, iliyojengwa kwa zaidi ya Sh584.2 milioni kupitia mpango wa Mpango wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Diwani wa Luchelele, Lipidius Mpanju, amesema ujenzi wa shule hiyo umepunguza umbali wa wanafunzi waliokuwa wakitembea zaidi ya kilomita tano kufuata masomo ya sekondari.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akitoa maelekezo baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa ghorofa tano katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ‘Butimba’ kwa gharama ya zaidi ya Sh14.015 bilioni. Picha na Saada Amir
Mtanda pia amekagua mradi wa ujenzi wa ghorofa tano ya hospitali katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ‘Butimba’ kwa gharama ya zaidi ya Sh14.015 bilioni, unaojumuisha huduma za dharura, mahtuti (ICU), maabara, mionzi, upasuaji, kliniki za macho na meno, wodi za wazazi na binafsi, pamoja na ofisi za utawala.
Mpaka sasa, mradi umefikia asilimia 83 ya utekelezaji, ukiwemo kumwaga zege kwa sakafu ya kwanza na kujenga kuta za boma.