Shinyanga. Kukumbatia wanyama wafugwao kama paka na mbwa ni jambo la kawaida kwa watu wengi, hususani watoto wanapocheza nao au vijana wanaowapeleka wanyama hao kupata tiba kwa wataalamu wa mifugo.
Licha ya ukaribu huo, wahusika wanaonywa kuhusu madhara ya kiafya, ikiwemo imani kuwa manyoya mepesi ya paka yanayopeperuka, yanaweza kusababisha ugonjwa wa pumu kwa binadamu pale yanapovutwa.
Hata hivyo, wataalamu wanabainisha kuwa kuna faida na hasara za kukumbatia wanyama hawa. Kazi mbalimbali za kitafiti zinaonyesha kuwa kuishi karibu na wanyama, husaidia kupunguza msongo wa mawazo, upweke, huzuni, kuboresha afya ya moyo, na kuwasaidia watoto kukuza kinga ya mwili mapema.
Lakini je, unajua kuwa kuna madhara makubwa ya kiafya yanayoweza kumpata binadamu anayekumbatia paka au mbwa asiyetunzwa?
Daktari wa mifugo kutoka Manispaa ya Kahama, Dk Damian Kilyenyi anasema kuwa asilimia 75 ya magonjwa yanayompata binadamu yanatoka kwa wanyama , hususan paka na mbwa ambao hawajapatiwa chanjo stahiki.
“Mtu anapofuga mifugo hii lazima ajue kuwa wanahitaji kutunzwa, kutibiwa na kupewa chanjo ili mfugaji awe salama kutokana na magonjwa,” anasema.
Kichaa cha mbwa na tishio la vifo
Dk Kilyenyi anabainisha kuwa ugonjwa ambao ni rahisi kuwapata watu wengi ni kichaa cha mbwa. Hii inasababishwa na wafugaji kukiuka Sheria namba 19 ya mwaka 2008 inayohusu haki na ustawi wa wanyama, hivyo kufuga kiholela na kuacha wanyama wakizurura mtaani bila chanjo.
Anasema chanjo ya kichaa cha mbwa hutolewa kabla ya mnyama kuugua, na akishapata ugonjwa huo hakuna tiba zaidi ya kumuua ili asisababishe madhara kwa viumbe wengine.
Kwa binadamu, anasema chanjo lazima itolewe mara moja baada ya kung’atwa, kwani kuchelewa kunaweza kusababisha kifo.
“Chanjo moja kwa mtu aliyeng’atwa na mbwa mwenye kichaa ni Sh35,000 na zinatakiwa dozi sita, sawa na Sh 175,000. Gharama hii ni kubwa kwa mwenye kipato cha chini, hivyo inaweza kusababisha kifo. Jamii iwe makini na kufuata sheria,” anasisitiza.
Aidha, daktari huyo anasikitishwa na uwepo wa mila potofu, ambapo baadhi ya watu huamini kurogwa na kuwakimbiza kwa waganga wa kienyeji wanafamilia waliong’atwa na mbwa badala ya kuwapeleka hospitali, jambo linalopoteza maisha ya wengi.
Kinga dhidi ya pumu, mzio na vimelea
Kuhusu hofu ya pumu, Dk Kilyenyi anathibitisha kuwa manyoya ya paka asiyechanjwa, yanaweza kuwa kichocheo cha ugonjwa huo kwa watu wanaomzunguka.
“Paka ana manyoya laini yanayonyonyoka kwa urahisi. Akitibiwa vizuri na kupewa chanjo, hakuna madhara hata ukimkumbatia, na hicho ndicho tunachohamasisha,” anasema.
Pia, mnyama asiyetunzwa anaweza kueneza magonjwa mengine kama minyoo, fangasi, bakteria na mzio unaosababisha kikohozi, kupiga chafya, na macho kuwasha kupitia mate au ngozi. Vimelea kama kupe na viroboto pia ni tishio kwa afya ya mfugaji.
Dk Kilyenyi anashauri kuwa, ili kuepuka madhara, ni muhimu kunawa mikono kwa sabuni baada ya kumshika mnyama, kuhakikisha mhusika anapata chanjo zote na kuepuka kuwabusu wanyama mdomoni.
Anasema kuwa kukumbatia mnyama si hatari ikiwa usafi na matunzo vitazingatiwa… “Kwa uangalifu na elimu sahihi, inawezekana kufurahia urafiki na wanyama bila kuhatarisha afya.”
Ili kufurahia urafiki na paka au mbwa wako bila kuhatarisha afya ya familia yako, wataalamu wanashauri yafuatayo:
Mosi, ulazima wa chanjo. Hakikisha mnyama anapata chanjo zote muhimu, hususan ya kichaa cha mbwa, kabla hajapata maambukizi.
Pili, usafi wa mikono. Nawa mikono yako kwa maji tiririka na sabuni kila mara baada ya kucheza na au kumshika mnyama.
Tatu, epuka kubusu. Tabia ya kuwabusu wanyama mdomoni, inaweza kusababisha maambukizi ya vimelea na bakteria kupitia mate.
Nne, tiba ya vimelea. Hakikisha mnyama anapewa dawa za minyoo, kupe, na viroboto mara kwa mara chini ya maelekezo ya daktari.
Tano, zingatia sheria: Fuata Sheria ya Haki na Ustawi wa Wanyama ya mwaka 2008, kwa kufuga mnyama katika mazingira yanayoeleweka badala ya kumuacha azurure.
Sita, wahi hospitali. Ikitokea umeng’atwa au kukwaruzwa, nenda kituo cha afya mara moja badala ya kwenda kwa waganga wa kienyeji.
Saba, matunzo ya manyoya. Hakikisha paka anapata matibabu sahihi ili kuzuia manyoya yake kuwa chanzo cha mzio au pumu.