WAKATI kikosi cha Yanga kikiendelea na mazoezi usiku huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar mdhamini wa timu hiyo Ghalib Said Mohamed (GSM), ameibuka mazoezi hapo.
Iko hivi; Yanga ilianza mazoezi saa 1 kamili jioni ikiwa na wachezaji wote akikosekana Mohamed Damaro ambaye hatakuwepo kutokana na adhabu ya kadi za njano.
Katikati ya mazoezi GSM alitinga saa 1:20 usiku akiongozana na familia yake ambayo ilikuwa jukwaani kushuhudia timu hiyo ikijifua.
Baada ya kufika mfadhili huyo ambaye inadaiwa amewaahidi wachezaji kiasi cha Sh1.2 bilioni aliketi mbele karibu kabisa na uwanja akiteta jambo na baadhi ya viongozi akiwemo Mratibu wa Yanga Princess, Kibwana Matokeo.
Lakini kabla ya GSM kufika viongozi wengine waliowahi mapema tangu timu inaanza mazoezi ni rais wa Yanga, Hersi Said na makamu wake, Arafat Haji.
Yanga itakuwa na mechi ya kufa au kupona Jumapili uwanjani hapo ikiikaribisha JS Kablyie ya Algeria kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.