TLS yampa mchungaji Malisa mawakili watano

Arusha. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimempa Mchungaji Godfrey Malisa anayekabiliwa na kesi mbili ikiwamo ya uhaini, uwakilishi wa jopo la mawakili watano.

Mbali na kesi ya uhaini, Malisa anakabiliwa na kesi nyingine ya makosa ya kimtandao iliyoanza kusikilizwa jana Februari 12,2026 na Hakimu Mkuu Mkazi, Ally Mkama wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Akizungumza na Mwananchi  leo Ijumaa Februari 13,2026, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, ametaja jopo la mawakili hao kutoka Chapter ya Kilimanjaro ni Leonard Mashabara, Deogratias Matata, Elisante Kimaro, Moonlight Tupa na Fredy Kimaro.

“Kwa pamoja jana wameingia katika shauri la jinai Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi linalomkabili ndugu Godfrey Malisa,” amesema.

“Shauri hilo lipo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mkama, liliendelea katika hatua ya usikilizwaji na shahidi mmoja wa upande wa mashtaka aliweza kutoa ushahidi wake na hatimaye kesi imeahirishwa hadi Februari 20,2026 ambapo itaendelea na usikilizwaji,” ameongeza Wakili Mwabukusi

Juzi Februari 11,2026 shauri hilo lilikwama kusikilizwa baada ya Malisa kuomba Mahakama iahirishe akisubiri msaada wa kisheria kutoka TLS, ombi ambalo lilikubaliwa na Mahakama kwa masharti kuwa juhudi za kuhakikisha mshtakiwa anapata uwakilishi zifanyike ili kesi ianze kusikilizwa.

Hakimu Mkama alimweleza mshtakiwa huyo kuwa hilo ni ahirisho la mwisho na kuwa kesi lazima ianze kusikilizwa Februari 12,2026 na kuwa siku hiyo Mahakama iliacha kusikiliza mashauri mengine ya madai matano ili isikilize kesi hiyo.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa maombi ya Malisa kupewa msaada wa kisheria yaliwasilishwa Februari 10,2026 hivyo, TLS Kilimanjaro, iliwasiliana na makao makuu ili ipate idhini na mawakili watakaomwakilisha.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 28411/ 2025, Malisa anatuhumiwa kuchapisha taarifa kwenye mtandao wake wa YouTube, akimdai Rais Samia Suluhu Hassan, anatakiwa kujiuzulu kwa kusimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.

Katika kosa la kwanza, upande wa mashitaka unadai kuwa mchungaji Malisa alitenda kosa hilo Novemba 15,2025 huko Miembeni katika Wilaya ya Moshi na alichapisha maneno hayo katika akaunti ya YouTube yenye jina Godfrey Malisa.

Hati ya mashitaka, inanukuu maneno aliyoyachapisha kuwa: “Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.”

Upande wa Jamhuri unadai alichapisha maneno hayo akijua fika kuwa taarifa hizo hazikuwa sahihi na zilikuwa na lengo la kupotosha umma wa Watanzania.

Katika kosa la pili, anatuhumiwa kufanya uchochezi kinyume na kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Maelezo ya kosa ni kuwa Novemba 15,2025 huko Miembeni Wilaya ya Moshi, anadaiwa kuchochea umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda kosa la jinai ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria.

Mbali na kesi hiyo, mchungaji Malisa anakabiliwa na kesi ya uhaini chini ya kifungu 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali hapa Tanzania.