WAKATI Yanga ikijiandaa na mechi ya mwisho ya Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, kuna ishara kuwa mabingwa hao wa Tanzania hawataki kuacha jambo.
Yanga inahitaji ushindi wa zaidi ya bao moja ili kukata tiketi ya kwenda robo fainali, huku ikisikilizia matokeo ya mechi kati ya Al Alhy na AS Far Rabat.
Mazoezi ya usiku huu, beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye aliyeiteka shoo akitoa krosi za maana na kufunga mabao.
Katika mazoezi ya kumalizia mashambulizi, mchezaji huyo amefunga mabao matatu kati ya asisti tano alizopewa akiwa na ufanisi wa hali ya juu.
Kwa lugha rahisi ni kwamba makocha Yanga wanaweza kucheza kwa kushambulia kuanzia nyuma.
Katika mechi ambayo lazima upate mabao ya kutosha, mabeki wa pembeni hugeuka kuwa washambuliaji wa ziada, kwani kupanda kwao mbele huongeza idadi ya wachezaji ndani ya boksi la timu pinzani.
Kuna dalili zinaonyesha huenda mechi hiyo Tshabalala akapewa uhuru wa kupanda, akifanya mikimbio mara kwa mara na kuvunja safu ya ulinzi ya JS Kabylie.