Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wametaka kuandaliwa kwa sheria mpya itakayosaidia elimu nchini, ambayo pamoja na mambo mengine itaimarisha uwajibikaji, usimamizi, elimu jumuishi na mifumo ya tathmini ili kuendana na mabadiliko ya sera, mitaala na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa sasa, sekta hiyo inasimamiwa na Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, ambayo inaelezwa kuwa imepitwa na wakati, hivyo kunahitajika sheria mpya itakayoendana na hali ya sasa.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa katika kikao cha mapitio ya Sheria ya Elimu, kilichowakutanisha wawakilishi wa Serikali na mashirika ya kiraia chini ya uratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET).
Mwenyekiti wa kamati ya mapitio ya Sheria ya Elimu, Profesa Saudin Mwakaje, amesema kamati hiyo iliyafikia makundi mbalimbali ya wadau katika sekta ya elimu, waliotoa mapendekezo kadhaa ambayo yanaonesha kinachohitajika kufanyika sasa si maboresho, bali kuandaliwa kwa sheria mpya.
Amesema kutokana na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, ipo haja ya kuwa na sheria itakayoendana na yaliyomo kwenye sera hiyo na kufanikisha utekelezaji wa ya Taifa ya Maendeleo.
“Sheria ya sasa ina mapungufu mengi, sasa wadau wamependekeza kutokana na mapungufu hayo, sera tuliyonayo sasa na malengo ya shabaha za Dira ya 2050, kuna haja ya kuwa na sheria mpya ya elimu na siyo kuifanyia maboresho,” amesema Profesa Mwakaje.
Miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa ni uwajibikaji na usimamizi katika sekta ya elimu, ambapo wadau hao wamebainisha kuwa sheria ya sasa ina mianya inayosababisha ukosefu wa uwazi katika majukumu ya taasisi na mamlaka mbalimbali zinazosimamia elimu.
Eneo lingine lililopendekezwa na wadau kwenye kamati hiyo ni elimu jumuishi kupewa kipaumbele, ambapo msisitizo ni kuwekwa kwa misingi madhubuti ya elimu jumuishi ndani ya sheria.
Pamoja na sera kuelekeza kuwa hakuna mtoto anayeachwa nyuma, bado utekelezaji unakabiliwa na changamoto kutokana na ukosefu wa vifungu vinavyolazimisha upatikanaji wa miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Wadau wametaka sheria itamke bayana wajibu wa Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha watoto wenye ulemavu, wanaotoka mazingira magumu na makundi mengine maalumu wanapata haki sawa ya elimu bora.
Aidha, wamependekeza kuwe na utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha takwimu za watoto walio nje ya mfumo wa elimu zinakusanywa na kufanyiwa kazi kwa ufanisi.
Katika mazingira ya ufundishaji, wadau wamependekeza maboresho ya sheria yanapaswa kuzingatia miundombinu ya shule, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na rasilimali watu.
Eneo lingine lililopendekezwa kufanyiwa kazi kisheria ni kuanzishwa kwa mifumo bora ya tathmini na ufuatiliaji wa ubora wa elimu.
Kuendana na mabadiliko ya kijamii na kiteknolojia, wadau hawakuacha kugusia mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea duniani, ambapo mapendekezo ni sheria kutambua matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, ikiwemo elimu kwa njia ya mtandao, ili kuweka msingi wa kisheria unaoendana na zama za kidijitali.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mratibu wa TEN/MET, Martha Makala, amesema mchakato huo umehusisha ukusanyaji wa maoni, mijadala ya kitaalamu na uchambuzi wa kina wa changamoto zilizopo katika utekelezaji wa sheria ya sasa.
Amesema mapitio hayo yamelenga kuhakikisha kuwa Sheria ya Elimu inaendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, pamoja na maboresho ya mitaala na nyaraka nyingine muhimu za elimu; lengo likiwa ni kuweka uwiano kati ya sera, sheria na utekelezaji wake kwa vitendo.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amewashukuru wadau kwa ushiriki wao, akisema uwepo wa sauti mbalimbali ni ishara ya uongozi unaosikiliza na kuthamini maoni ya wananchi katika maboresho ya sekta ya elimu.
“Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha mageuzi ya elimu yanatekelezwa kikamilifu kama ilivyokusudiwa, hivyo, nawasihi muendelee kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kwa pamoja tuweze kupata matokeo chanya ya mageuzi haya,” amesema Wanu.