WIZARA YA ARDHI KUANZISHA KLINIKI MAALUM YA WANAWAKE

Na Munir Shemweta, WANMM

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaendesha Kliniki Maalum ya Ardhi kwa ajili ya wanawake itakayojulikana kwa jina la “Samia Ardhi Week.”

Kiniki hiyo itashughulikia changamoto za ardhi kwa wanawake na itafanyika kuanzia tarehe 2 hadi 7 Machi 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo huadhimishwa tarehe 8 Machi kila mwaka ambapo kwa mwaka huu inaongozwa na Kaulimbiu “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050”

Akizungumza jijini Dodoma tarehe 12 Februari 2026 wakati wa kuahirisha Kliniki Maalum ya Maombi ya Hati, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amesema, wanawake wote wenye changamoto za ardhi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo kliniki hizo zitafanyika.

“Wanawake wote wenye shida za masuala ya ardhi wanatakiwa kujitokeza katika mikoa ya Tanzania Bara ambayo kliniki hizo zitafanyika” amesema Mhe Dkt. Akwilapo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nia ya wizara yake kuanzisha kliniki za ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ni kuwafikia wananchi wenye shida zinazohusiana masuala ya ardhi.

Akizungumzia Kliniki Maalum ya Maombi ya Hati aliyoiahirisha, Mhe. Dkt Akwilapo amesema, kliniki hiyo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo hadi kufikia tarehe 12 Februari 2026 wananchi 4,597 wamehudumiwa huku Hatimilki 3,878 zikiwa zimeandaliwa.

“Kumbe kupata hati inawezekana, katika hati 3,878 zilizoandaliwa jumla ya hati 1,508 zimechukuliwa na wahusika huku hati 2,370 zikiwa bado hazijachukuliwa”, amesema Dkt. Akwilapo.

Ametoa rai kwa wananchi ambao wamepata huduma na hati zao zimekamilika wafike ofisi za ardhi kwa ajili ya kuzichukua kwa kuwa hati hizo za ardhi ni mali yao.

Kliniki Maalum ya Maombi ya hati ilianza januari 28, 2026 katika viwanja vya Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma na kuhitimishwa tarehe 12 Februari 2026.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa kuahirisha Kliniki Maalum ya Maombi ya Hati iliyoanza januari 28, 2026 na kuhitimishwa Februari 12, 2026 jijini Dodoma.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi hati milki ya ardhi mmoja wa wananchi wa jiji la Dodoma aliyepata huduma katika kliniki maalum ya maombi ya hati tarehe 12 Februari 2026.

Sehemu ya wananchi wa jiji la Dodoma waliojitokeza kupata huduma katika Kliniki Maalum ya Maombi ya Hati wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (hayupo pichani ) wakati wa kuahirisha kliniki hiyo tarehe 12 Februari 2026.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya akizungumza wakati wa kuahirisha kliniki Maalum ya Maombi ya hati iliyofanyika katika Ofisi za Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akizungumza wakati wa wa kuahirisha kliniki Maalum ya Maombi ya hati iliyofanyika katika Ofisi za Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)