Dk Mwigulu ashtukia ‘kichaka cha gharama’, asema…

Tanga/Dar. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameendelea kukunjua makucha baada ya kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, kwa kile alichokiita ‘kichaka cha gharama’ kinachotumiwa kuhalalisha upotevu wa fedha za umma.

Dk Mwigulu ametoa maagizo hayo leo, Jumamosi, Februari 14, 2026, akiwa wilayani Kilindi, Mkoa wa Tanga, katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo aliyoanzia jana. Anakagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Jana, Ijumaa, akiwa akiweka jiwe la msingi na kukagua kituo cha kupoza umeme cha Mkata, alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuhakikisha ifikapo mwisho wa mwezi huu, fedha za ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Imani, Mkata Magharibi, ziwe zimefika.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkata Magharibi, Mussa Ngana, aliwasilisha ombi la kusaidiwa kutokana na uchakavu wa madarasa matatu ya shule hiyo, ambayo kwa sasa hayatumiki.

Majengo ya Hospitali ya Wilaya Kilindi iliyojengwa kwa gharama ya Sh2.64 bilioni.



“Muandikie kabisa Katibu Mkuu kwamba mwisho wa mwezi fedha iwe imefika. Mkurugenzi anasikia na Mkuu wa Mkoa pia. Fedha itoke popote pale, wakate safari na matumizi yasiyo ya lazima, kila mtu anywe chai nyumbani kwake, fedha hiyo ije tutengeneze kizazi cha kesho hapa,” amesema Dk Mwigulu.

Leo, Jumamosi, akiwa Kilindi, Dk Mwigulu amesema hatavumilia mbinu za kupandisha gharama za miradi kwa kisingizio cha ununuzi wa vifaa kutoka mbali wakati vinapatikana katika maeneo husika.

Katika ziara hiyo, Dk Mwigulu amesema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa hospitali ya wilaya aliyoweka jiwe la msingi, lakini akaibua maswali kuhusu idadi ya majengo yaliyojengwa kulinganisha na fedha zilizotolewa.

“Nimeambiwa fedha iliyokuja ilitakiwa ijenge majengo tisa, lakini mmejenga majengo pungufu. Fedha nyingine mmepeleka wapi?” amehoji.

“Kamanda wa Takukuru (Mkoa wa Tanga), fanyia uchunguzi wa hiki chote kilichofanyika, niipate hiyo taarifa niweze kuchukua hatua. Hatuwezi kuruhusu vichaka. Nikigundua gharama imepanda kwa kwenda kufuata vifaa mbali, nitachukua hatua kali za kinidhamu na kisheria,” amesema Dk Mwigulu.

Ametolea mfano wa mradi wa Veta mkoani Tanga, ambako alibaini kuwepo kwa mifuko 1,200 ya saruji iliyoganda ilhali mkoa huo una viwanda vya kuzalisha saruji.

“Jana nilipita pale nikasemea jambo la Veta, wakiwa wamegandisha mifuko wakati Tanga kuna viwanda vya saruji. Inakuwaje saruji ya kujengea Tanga itoke Dar es Salaam au Mbeya?” amehoji.

Amesema tabia ya kupandisha gharama zisizo na msingi inaibebesha Serikali mzigo usio wa lazima na kuathiri utoaji wa huduma katika maeneo mengine, huku baadhi ya watumishi wakijificha kwenye kisingizio cha tofauti za bei.

“Mnajificha kwenye kichaka cha gharama. Mnafikiri nimekuja kutembea? Niko kazini, nina taarifa zote,” amesema.

Mbali na hospitali ya wilaya, Dk Mwigulu ameagiza uchunguzi maalumu kufanyika katika ujenzi wa zahanati baada ya kubaini fedha kiasi cha Sh50 milioni matumizi yake hayaeleweki.

“Pale kwenye zahanati zilikuja Sh50 milioni, naambiwa zimetumika kupakapaka rangi. Naagiza Takukuru iwafuatilie wahusika wote walioshiriki, hata kama walishahama, kulekule waliko wachunguzwe, fungueni mashtaka, na ikionekana wana hatia, fukuzeni,” amesema.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi wa Kilindi leo Februari 14, 2026 baada ya kuweka jiwe la msingi la Hospitali hapo.



Amesisitiza haiwezekani fedha za umma zielekezwe kwenye miradi ya afya inayolenga kuhudumia wananchi kisha zitumike kwa kazi zisizoendana na thamani ya fedha iliyotolewa.

“Wafuatilie wote waliohusika na ujenzi huu wa zahanati. Hatuwezi kuwa na utaratibu watu wana uhitaji wa zahanati, fedha inakuja inatumika tofauti na mipango. Tunataka watu wanufaike na rasilimali. Jitihada anazofanya Rais watu wazione, zisinufaishe wachache,” amesema.

Amesema hatasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi watakaobainika kupindisha matumizi ya fedha au kuongeza gharama kwa makusudi, akieleza kuwa lengo la Serikali ni kuona wananchi wananufaika na rasilimali za Taifa.

Mbali na masuala ya matumizi ya fedha, Waziri Mkuu pia amezungumzia migogoro kati ya wakulima na wafugaji, akisisitiza makundi hayo ni ndugu na mhimili wa uchumi wa Taifa.

Katika kukabiliana na hilo, ameagiza mawaziri wa wizara sita kukutana Februari 16, 2026, mkoani humo na kuyaainisha maeneo yote yenye migogoro, kisha kuitafutia suluhisho la kudumu. Wizara hizo ni Maliasili na Utalii, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maji na Tamisemi.

“Hatuwezi kutenganisha jamii hizi. Tusifikishwe mahali mkulima akimuona mfugaji anaona adui yake. Tukifika hapo, hatutakuwa na Taifa. Suluhisho si kugombana, hata tukigombana ardhi haiongezeki, tunachotakiwa kufanya ni kupanga matumizi bora ya ardhi.

“Msigombane kuhusu mipaka, tumieni wazee wenu na sisi Serikali tutatumia wataalamu wetu kuja kuyamaliza. Shida ni kwamba kuna viongozi wakipewa rushwa wanaharibu mipango ya eneo husika, hili halikubaliki,” amesema.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba leo Februari 14, 2026 ameweka jiwe la msingi la Hospitali ya Wilaya Kilindi iliyojengwa kwa gharama ya Sh2.64 bilioni.



Kauli hiyo ya Waziri Mkuu imekuja baada ya wananchi kuibua kero ya migogoro ya ardhi na mipaka kati ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, huku kukiwa na matukio ya wakulima na wafugaji kuingia kwenye migogoro inayosababishwa na matumizi ya ardhi.

Amesema kwa miaka mingi jamii hizo zimeishi kwa kushirikiana, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakivunja sheria kwa makusudi, ikiwamo kuingiza mifugo katika mashamba ya watu bila ridhaa.

“Ni kinyume cha sheria mtu kwenda kuchunga kwenye shamba la mtu. Lakini msichukue sheria mkononi; Serikali itachukua hatua,” amesema.

Akikumbusha tukio alilowahi kukutana nalo mkoani Morogoro, Dk Mwigulu amesema aliwahi kuagiza kukamatwa kwa wahusika baada ya mfugaji kumshambulia mkulima kwa mkuki kufuatia mgogoro wa mifugo kuingia shambani.

“Niliagiza RPC akamate wote isipokuwa wajawazito, ili tuwaoneshe Serikali ipo,” amesema.

Alichokisema mbunge, Aweso

Akizungumza kwenye ziara hiyo, mbunge wa Kilindi (CCM), Salehe Mhando, ameeleza changamoto ya miundombinu ya barabara, akieleza kuwa kiu ya wakazi wa jimbo hilo ni kuona barabara ya lami kutoka Handeni hadi makao makuu ya Wilaya ya Kilindi.

“Kwa niaba ya wazee wangu na wana Kilindi wote, niombe ilani yetu itimizwe, maana barabara hii ipo kwenye ilani ya uchaguzi. Tunataka tuutengeneze mji wa Kilindi kuvutia uwekezaji, na hata wafanyakazi wakipangiwa huku basi waone ni eneo sahihi la kufanyia kazi.”

Kuhusu changamoto ya maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amekiri wizara yake inatambua changamoto hiyo katika eneo hilo, akieleza kuwa tayari zilifanyika jitihada za kuitatua, moja wapo ikiwa ni kuchimba visima.

“Baada ya kubaini hapa kuna changamoto ya maji chini ya ardhi, tukakaa na wataalamu na kukubaliana lazima jitihada zote zifanyike tupate maji. Tuliwashirikisha wazee na visima vikachimbwa, maji yakapatikana, kinachofuata sasa kuyafikisha hayo maji kwa watu. Tutaleta Sh500 milioni kwa ajili ya kazi hiyo.

“Mbali na hilo, kilomita 76 kutoka hapa kuna mto Dibuluma, ambao upo Mvomero. Tunaenda kutekeleza mradi wa maji ambao utasaidia pia kuleta maji kwenye vijiji vya Kilindi,” amesema Aweso.