Zanzibar. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Abdulah amesema maadhimisho ya Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki (EAC) yametoa nafasi ya kutafakari maendeleo ya Kiswahili katika jumuiya hiyo.
Amesema hayo leo Jumamosi, Februari 14, 2026 wakati akiwasilisha salamu za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi.
Hemed ametoa wito kwa nchi wanachama kuhakikisha wanaweka mkazo katika kuanzisha mabaraza ya Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki (EAC).
Amesema Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki (Kakama) inalo jukumu la kuhakikisha inawahusisha vyama mbalimbali na wadau wake katika maendeleo ya Kiswahili.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amewatakia wananchi salamu za upendo kutoka kwa Rais Samia wanapoadhimisha Siku ya Wapendanao maarufu Valentine Day.
Ameipongeza Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki kwa juhudi za kusimamia Kiswahili na leo ikitimiza miaka 10.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Makonda, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema ni wakati mwafaka kwa kila nchi kuanzisha mabaraza ya Kiswahili.
Amesema Kakama inapoadhimisha miaka 10, pia Tanzania itakuwa na Kongamano la Kiswahili litakalofanyika Aprili mwaka huu nchini Ufaransa, hivyo lugha hiyo itaendelea kutangazwa.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania, Kenya na Uganda zinatarajiwa kuwa wenyeji wa mashindano ya Afcon mwaka 2027, hivyo ni wakati mwafaka kutumia fursa hiyo kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili duniani.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Afrika Mashariki, Dk Caroline Asiimwe amesema maadhimisho ya miaka 10 ya kamisheni hiyo yameonesha nia thabiti ya kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa nchi nane wanachama.
Amesema kwa takribani miaka kumi ya Kamisheni hiyo imewezesha kushirikisha wadau mbalimbali, kuhimiza sera pamoja na kufanya tafiti mbalimbali zilizosaidia maendeleo ya Kiswahili.
Amesema ufanisi wa Kakama umetokana na ushiriki wa kila nchi mwanachama huku akitoa wito wa kutafakari kwa kina miaka kumi ijayo.
Ametoa mwelekeo mpya wa kuangalia namna ya kuitumia akili unde (AI) kama fursa mpya katika kuendeleza Kiswahili kimataifa.
Dk Asiimwe amesema ni muhimu kuwekeza katika lugha ya Kiswahili na hata kutumia fursa ya kujifunza lugha zingine ili kuifanya Kiswahili kufika mbali zaidi.
Amesema hatua ya Kiswahili kutambuliwa kuwa lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo amehimiza utekelezaji wake kufanyika kwa dhati katika kila nchi.