Kigogo arejea Mbeya City na ujumbe, mashabiki mzuka

ALIYEKUWA Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Ally Nnunduma amesema licha ya timu hiyo kuanza msimu kwa matokeo yasiyoridhisha, lakini ina uwezo wa kumaliza kibabe Ligi Kuu Bara kutokana na mipango na mikakati ya ndani na nje ya uwanja.

Nnunduma aliiongoza Mbeya City kwa takriban misimu miwili akipokea nafasi ya mtangulizi wake, Emanuel Kimbe ambapo anakumbukwa zaidi kwa kuirudisha timu hiyo Ligi Kuu huku akiiacha timu hiyo katika nafasi nzuri.

Katika Ligi Kuu, Nnunduma aliyekuwa mchumi katika Jiji la Mbeya, alisimamia michezo minne ikishinda miwili dhidi ya Fountain Gate 1-0 na KMC 3-0, sare moja dhidi ya Yanga na kupoteza mbele ya Azam 2-0 akiiacha na pointi saba.

Kwa sasa kigogo huyo ni kaimu mkurugenzi katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu anayeshughulikia sera, utafiti na ubunifu, ambapo leo Februari 14 amefanya kikao maalumu na mashabiki na wachezaji wa timu hiyo na kuweka mipango ya kufanya vizuri.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nnunduma amesema lengo la kufanya kikao hicho ni kuweka mikakati mipya na kuazimia baadhi ya mambo yatakayoiwezesha timu hiyo kurejesha makali yake.

Amesema licha ya matokeo yaliyopita kutoridhisha, lakini kwa sasa upo mwelekeo mpya na baada ya kikao baina ya mashabiki, benchi la ufundi na wachezaji anaamini City itafanya vizuri.

“Nimeona nikutane nao tupange upya mikakati, viongozi wa timu kwa sasa wanafanya vizuri na kinachotakiwa ni ushirikiano, naamini kupitia kikao hiki tunaenda kuiona Mbeya City ya tofauti,” amesema Nnunduma.

Kwa upande wake, katibu wa mashabiki wa timu hiyo, Timoth Mwalongo ‘Mkandarasi’ amesema wataendelea kumkumbuka Nnduma kwa heshima aliyoweka haswa kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu.

Amesema kwa sasa mashabiki ni kuendelea kuisapoti timu hiyo kwa mechi zilizobaki kuanzia mchezo ujao wa kombe la shirikisho dhidi ya Biashara United kuhakikisha wanafanya vizuri.

“Tunamshukuru kuja kutuaga lakini mchango wake tutaendelea kuutambua, tumekuwa naye wakati wote na sisi mashabiki tutaendelea kuipa nguvu timu ili mechi zilizobaki tufanye vizuri,” amesema Mkandarasi.