Mikoa minne Tanzania kunufaika na mpango wa matumizi ya ardhi

Iringa. Katika kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi na maendeleo, vijiji 160 vya mikoa ya Iringa, Ruvuma, Njombe na Lindi inatarajiwa kunufaika na uandaaji wa mipango ya natumizi ya ardhi.

Ushirikiano huo unalenga kupunguza migogoro ya ardhi, kulinda misitu na bioanuwai, na kuongeza ushiriki wa jamii katika maamuzi yanayohusu rasilimali zao, huku wakinufaika kiuchumi na kijamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Hatua hiyo inakuja baada ya makubaliano hayo kusainiwa leo, Februari 14, 2026, Gangilonga Manispaa ya Iringa, yakilenga kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vilivyopo katika maeneo ya mradi.

Mkurugenzi Mkuu wa NLUPC, Joseph Mafuru, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo akisema: “Mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ni msingi wa maendeleo yenye mpangilio na usimamizi endelevu wa rasilimali zetu. Ushirikiano huu na Forland utaimarisha uwezo wa kitaalamu katika ngazi ya wilaya na kijiji na kuhakikisha mipango inakidhi viwango vya kitaifa na mahitaji halisi ya jamii.

“Kupitia makubaliano haya, tunatarajia kuona ongezeko la vijiji vyenye mipango iliyoidhinishwa, kupungua kwa migogoro ya ardhi, na kuimarika kwa ushiriki wa wananchi katika maamuzi yanayohusu rasilimali zao.”

Kupitia makubaliano ya kifedha na kiufundi, kutawezesha uandaaji wa mipango hiyo kufanyika kwa ufanisi, huku mwongozo wa kitaifa na usimamizi kitaalamu ukitolewa kupitia PLUM ili kuhakikisha ramani na upangaji wa ardhi unafanywa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji halisi ya jamii.

Mafuru amesema kuwa hali hiyo inatoa fursa kwa jamii kupanga kwa uwazi matumizi ya ardhi yao, iwe kwa kilimo, malisho, makazi au hifadhi ya misitu, huku ikihakikisha rasilimali za asili zinatunzwa na kufaidisha wananchi kiuchumi na kimaisha.

Kupitia makubaliano hayo, Forland itatoa msaada wa kifedha na kiufundi ili kuhakikisha mchakato wa upangaji unatekelezwa kwa ufanisi, huku NLUPC ikitoa mwongozo wa kitaifa na kusimamia kitaalamu mchakato huo kupitia timu za usimamizi wa matumizi ya ardhi.

Timu hizo za PLUM zitapatiwa mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha kuimarisha uwezo wao katika upangaji, uchambuzi wa rasilimali na uandaaji wa ramani za matumizi ya ardhi kwa kuzingatia viwango vya kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mtaalamu wa matumizi bora ya ardhi katika mradi wa Forland, Andrew Fednands, amesema ardhi ni rasilimali muhimu nchini, inayotumika kwa kilimo, misitu, makazi, utunzaji wa mazingira na shughuli nyingine za kiuchumi, na bila mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi, migogoro inaweza kuongezeka na rasilimali za asili kuharibika.

Fednands amesema mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji itasaidia jamii kuamua kwa uwazi namna ardhi yao itakavyotumika, iwe kwa kilimo, hifadhi ya misitu, malisho, makazi au matumizi mengine, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na baadaye.

“Forland itajikita katika kuendeleza shughuli za misitu, kutunza mazingira na kuainisha misitu ya hifadhi ya vijiji ili iweze kulindwa na kuwanufaisha wananchi kiuchumi, huku ikihifadhi bioanuwai na mifumo ikolojia,” amesema.

Aidha, Fednands amesema mipango hiyo itawezesha kutenga maeneo mengine ya matumizi, kupunguza migogoro ya ardhi na kusaidia upatikanaji wa hati miliki za kimila kwa wananchi wa vijijini.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, mshauri mkuu wa mradi wa Forland, Michael Hawkes, amesema: “Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kuimarisha upangaji endelevu wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya kijiji, na kwa kushirikiana kwa karibu na NLUPC na timu za wilaya, tunaziwezesha jamii kusimamia ardhi yao kwa kuzingatia matumizi endelevu, kupunguza migogoro, na kulinda rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.”

Aliongeza kuwa: “Kupitia mipango hii, tunataka kuona vijiji vinakuwa na dira ya wazi ya matumizi ya ardhi yao, vinanufaika kiuchumi na misitu yao, na wakati huohuo vikichangia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”

Wananchi katika baadhi ya vijiji vinavyotarajiwa kunufaika wamepokea ushirikiano huo kwa matumaini makubwa, wakieleza kuwa mipango ya matumizi ya ardhi itasaidia kuweka mipaka wazi kati ya maeneo ya kilimo, malisho na hifadhi ya misitu.

Mmoja wa wakazi wa Mkoa wa Njombe, Daudi Hassan, amesema: “Tunaamini mipango hii itasaidia kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji na kutupa uhakika wa matumizi ya ardhi yetu kwa maendeleo ya familia zetu.”

Mkazi mwingine kutoka Mkoa wa Lindi, Gwan Tais, ameongeza: “Kupata hati miliki ya kimila na kuwa na ramani ya kijiji itatupa usalama zaidi na kutuwezesha kuwekeza katika kilimo na misitu bila hofu ya kupoteza ardhi.”

Forland ni programu ya miaka minne, inayofadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Serikali ya Finland, na kutekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Misitu na Nyuki, ikiwa na lengo la kukuza usimamizi endelevu wa misitu, kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kukuza biashara jumuishi za misitu.

Ushirikiano huo wa Forland na NLUPC, kwa kipindi cha miaka minne ya mradi, unalenga kupunguza migogoro ya ardhi, kulinda misitu na bioanuwai, na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii za vijijini ili kuwanufaisha wananchi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.