Miracle Experience Balloon Safaris Yatwaa Tuzo ya Muendeshaji Bora wa Safari za Puto Tanzania

KAMPUNI ya utalii wa puto angani, Miracle Experience Balloon Safaris, imetajwa kuwa Muendeshaji Bora wa Safari za Puto Tanzania katika tuzo za Serengeti Awards zilizofanyika Desemba 19, 2025. Hafla hiyo iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kutambua mchango wa wadau wanaoendeleza sekta ya utalii nchini.

Tuzo hiyo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuweka viwango vya ubora wa huduma, usalama na uhifadhi wa mazingira, huku ikiitambua kampuni hiyo kwa mchango wake katika kukuza sifa ya Tanzania kama kitovu cha kimataifa cha utalii wa wanyamapori.

Timu ya uendeshaji ya kampuni ilipokea tuzo hiyo kwa niaba ya uongozi na kueleza fahari yao kwa mafanikio hayo.

Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Hasnain Sajan, alisema heshima hiyo ya kitaifa inaakisi miaka ya nidhamu ya kiutendaji na mipango makini. Alieleza kuwa tangu mwaka 2019 wamejikita kubadili taswira ya safari za puto juu ya mandhari maarufu za Tanzania kwa kutoa uzoefu salama, wa kipekee na unaomruhusu mgeni kuunganishwa na asili.

Tangu kuanzishwa kwake, kampuni hiyo imefanya zaidi ya safari 19,000 za puto na kubeba takribani abiria 80,000, ikiwa na wafanyakazi 280, magari 54 na puto 16. Mafanikio hayo yanaifanya kuwa miongoni mwa waendeshaji wakubwa wa safari za aina hiyo nchini.

Tuzo za Serengeti zinachukuliwa kuwa utambuzi mkuu wa ubora katika utalii, uhifadhi na urithi wa utamaduni Tanzania, zikihusisha kura za umma na tathmini za wataalamu kwa ushirikiano na Tanzania National Parks Authority. Lengo lake ni kuhamasisha ubunifu, uendelevu na utoaji wa huduma zenye viwango vya kimataifa katika mnyororo mzima wa thamani wa utalii.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, idadi ya watalii wa kimataifa ilifikia takribani milioni 2.16 katika mwaka ulioishia Aprili 2025, huku mapato ya utalii yakichangia karibu asilimia 56 ya mauzo ya huduma nje ya nchi, jambo linalothibitisha umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi na upatikanaji wa fedha za kigeni.

Katika tuzo za kimataifa za World Travel Awards mwaka 2025, Tanzania ilitangazwa kuwa Kivutio Kinachoongoza Barani Afrika, huku Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiendelea kushinda kama Hifadhi Bora Afrika. Vilevile, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ulitambuliwa kama uwanja bora Afrika, Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kama hifadhi yenye mandhari bora, na Zanzibar kuwa kitovu kinachoongoza kwa matukio na tamasha.

Kampuni hiyo imejenga sifa kupitia safari za puto zilizoidhinishwa zinazotoa mwonekano mpana wa ikolojia ya Serengeti, pamoja na huduma za kifahari chini ya mwavuli wa Miracle Collection, ikiwemo safari katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na eneo la Singita Grumeti. Serikali imesisitiza kuwa ukuaji wa utalii lazima uende sambamba na uhifadhi na usalama, huku utambuzi huo ukiashiria mchango wa kampuni katika kudumisha hadhi ya Tanzania kama moja ya vivutio vikuu vya safari duniani.