Licha ya kwenda mapumziko ikiwa nyuma Kwa mabao 2-0, Tanzania Prisons imefanya ‘comeback’ kwa kuizamisha Namungo 3-2 na kujihakikishia pointi tatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Mabadiliko ya kiufundi yaliyofanywa na Prisons kwa kumpumzisha George Mpole na kuingia Oscar Mwajanga yameonekana kuwalipa maafande hao na kuonja ushindi waliokosa kwa michezo tisa.
Katika mchezo huo uliopigwa leo Februari 14 katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Namungo ndio walitangulia kupata bao kupitia kwa Cyprian Kipenye kwa mpira wa penalti kisha Fabrice Ngoy kuweka la pili dakika ya 38.
Kipindi cha pili Lambart Sabiyanka aliipatia bao Prisons kisha Mpole kuingia wavuni huku Mwajanga aliyetokea benchi akaiongezea la tatu na kuihakikishia ushindi huo walioukosa kwa dakika 720 na kumuweka kwenye wakati mgumu kocha Mkuu wa timu hiyo, Zedekiah Otieno.
Huo unakuwa ushindi wa tatu kati ya michezo 14 waliyocheza Prisons, huku wakipoteza saba na sare tatu na sasa wanachumpa hadi nafasi ya 12 kwa pointi 12.
Hata hivyo, Namungo watajilaumu baada ya kukosa penalti baada ya Kipenye kupaisha mpira na kufanya wenyeji kuongeza nguvu na ari kiko na kubaki na ushindi huo, na kuchaguliwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kocha msaidizi wa Prisons, Innocent Mwangonde amesema ushindi huo unaamsha morali na kupunguza presha kwa wachezaji akieleza kuwa kazi imeanza.
“Mabadiliko ya kumtoa Mpole tuliona amekata pumzi, tukamuona Mwajanga anaweza kuwasumbua mabeki na akaweza kufanya tulichotarajia. Tunaenda kusahihisha makosa yaliyoonekana,” amesema Mwangonde.
Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema walikosa umakini na kuwapa wapinzani wao nafasi kupata bao la ushindi akiahidi kufanyia marekebisho upungufu.
“Tumefanya makosa tumeadhibiwa, penalti tuliyokosa ilitupunguza nguvu ila nampongeza mchezaji kwa kuwa alionyesha kiwango bora, hiyo ni sehemu ya mpira tunaenda kujisahihisha,” amesema Mgunda.