Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria barani Afrika yanahitaji uongozi na usimamizi thabiti wa Waafrika wenyewe, umiliki wa kweli wa programu zake pamoja na dhamira ya kisiasa ya muda mrefu.
Amesema vita dhidi ya malaria si suala la afya pekee, bali ni ajenda ya maendeleo, uchumi na ustawi wa rasilimali watu barani Afrika.
Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Februari 14, 2026, wakati akishiriki katika mkutano wa ngazi ya juu na vyombo vya habari uliolenga kujadili ufadhili endelevu wa mapambano dhidi ya malaria barani Afrika, pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika makao makuu ya Umoja huo, jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Rais Samia amesema vita dhidi ya malaria si suala la afya pekee, bali ni ajenda ya maendeleo, uchumi na ustawi wa rasilimali watu barani Afrika.
“Mapambano dhidi ya malaria barani Afrika yanahitaji uongozi na usimamizi thabiti wa Waafrika wenyewe, umiliki wa kweli wa programu zake na dhamira ya kisiasa ya muda mrefu,” amesema.
Akieleza uzoefu wa nchi katika mapambano dhidi ya malaria, Rais Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika ajenda ya kutokomeza malaria.
Hiyo ni pamoja na kuwa mwenyeji wa African Leaders Malaria Alliance (ALMA) kama taasisi ya kuratibu mapambano hayo barani Afrika, iliyojengwa juu ya mifumo madhubuti ya uwajibikaji, pamoja na uwezo wa utekelezaji unaolenga matokeo.
ALMA ni muungano wa wakuu wa nchi wa Afrika unaolenga kuharakisha kutokomeza malaria na kuimarisha mifumo ya afya.
“Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa katika tafiti za kisayansi na ubunifu kupitia Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), ikiwemo utafiti wa teknolojia za kisasa za kudhibiti maambukizi ya malaria,” amesema.
Amebainisha jitihada za Tanzania za kuongeza matumizi ya vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu wanaoeneza malaria, chanjo za malaria, pamoja na kuboresha mifumo ya matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa kama miongoni mwa njia zilizotumika.
“Serikali imeimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kuhakikisha afua za malaria zinaunganishwa kikamilifu katika mfumo wa huduma za afya ya msingi na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo,” amesema.
Katika kuimarisha ufadhili wa ndani, Rais Samia amesema kupitia mabaraza ya kutokomeza malaria ya Tanzania Bara na Zanzibar, Serikali imeendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za dini, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kwenye uhamasishaji wa rasilimali za ndani kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria.
Ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, akieleza kuwa pamoja na jitihada za ndani, taasisi za kimataifa na washirika wa maendeleo wanapaswa kutekeleza ahadi zao kikamilifu na kwa wakati, hususan katika kuimarisha Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Malaria (The Global Fund) pamoja na matumizi ya rasilimali za Benki ya Dunia kwa ajili ya programu za malaria.
“Jitihada za kutokomeza malaria zinahitaji mshikamano wa pamoja wa nchi wanachama, ufadhili endelevu na matumizi ya takwimu sahihi katika kufanya uamuzi, pamoja na ubunifu unaozingatia mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa Botswana na Mwenyekiti wa ALMA, Duma Gideon Boko, amesema kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Malaria Barani Afrika ya mwaka 2025, Afrika bado ipo mbali kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.
Ripoti hiyo ya maendeleo ya malaria Afrika 2025 inaonesha kuwa Afrika bado inabeba zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi na vifo vya malaria duniani, huku kasi ya kutokomeza ikipungua.
“Nazihimiza nchi wanachama kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria, kuanzisha mabaraza ya kutokomeza malaria, pamoja na kutumia mifumo ya takwimu ili kuboresha utekelezaji,” amesema.
Naye Kamishna wa Afya, Masuala ya Binadamu na Maendeleo ya Jamii wa AU, Balozi Amma Iwum-Amoah, amesema kupungua kwa ufadhili wa kimataifa katika miaka ya karibuni kumeathiri juhudi za nchi mbalimbali za kupambana na malaria.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mabadiliko ya mtazamo katika ufadhili, uhimilivu wa mifumo ya afya dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya malaria.MWISHO