SERIKALI YAONGEZA USHIRIKIANO NA WADAU

Na Mwandishi wetu – Dodoma
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa mahusiano nchini kwa lengo la kutambulisha jukumu la sekta hiyo na kukusanya maoni yatakayosaidia kuandaa na kuboresha nyaraka za uimarishaji wa mahusiano.
Akizungumza Februari 13, 2026 jijini Dodoma wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu imefungua milango kwa wadau wote wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini na vyama vya siasa ili kushirikiana katika kujenga taifa lenye mshikamano.
“Tumekutana kujadili namna ya kuimarisha mahusiano na kuendeleza ushirikiano. Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unategemea amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa,” alisema Sangu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Jasper Makala, aliishukuru Serikali kwa kuitambua na kuiheshimisha sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali, akisema ziara hiyo imeimarisha mazungumzo na ushirikiano kati ya Serikali na sekta hiyo.
Amesema NaCoNGO itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kulinda amani na kusimamia maadili kupitia mifumo yao ya ndani, ili kuhakikisha mashirika wanachama yanafuata miongozo na taratibu zilizowekwa.