VIDEO: Familia tano zabaki bila makazi baada ya ajali ya moto Moshi

Moshi. Familia tano zimebaki bila makazi baada ya moto kuteketeza nyumba ya wapangaji yenye vyumba sita katika Mtaa wa Kanisani, Kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Gadafi Dauda Masudi amesema tukio hilo limetokea leo Jumamosi  Februari 14, 2026 asubuhi lakini halikusababisha madhara kwa kibinadamu.

Mwananchi Digital ilifika hadi eneo la tukio na kushuhudia wakazi wa mtaa huo wakifanya jitihada za awali za kuuzima moto kwa kutumia ndoo za maji kabla ya kufika kwa Zimamoto.

Hata hivyo moto ulikuwa tayari umeenea ndani na  juu ya paa, hivyo na juhudi hizo hazikuweza kuzaa matunda.

“Tulipokea taarifa saa 2:15 asubuhi na kupeleka magari mawili ya Zimamoto. Tulipofika tulikuta moto ukiendelea kuwaka, tukafanikiwa kuuzima na kuokoa zaidi ya nyumba tatu zilizokuwa hatarini kushika moto,” amesema Masudi.

Amesema mali zote zilizokuwa ndani ya vyumba vya wapangaji zimeteketea na chanzo cha moto bado kinachunguzwa kutokana na uwepo wa matumizi ya umeme na gesi ndani ya nyumba hiyo.

Nyumba ya wapangaji iliyopo Mtaa wa kanisani,kata ya Bomambuzi, Manispaa ga Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kuteketea kwa Moto. Picha na Yese Tunuka



“Tumekusanya vielelezo mbalimbali, baada ya uchunguzi kukamilika tutatoa taarifa rasmi ya chanzo cha tukio,” amesema Masudi.

Mmoja wa ndugu wa wamiliki wa nyumbani hiyo ya familia, Omega Msangi amesema tukio hilo limeishtua familia baada ya kupata taarifa saa tatu asubuhi na kushindwa kuokoa mali yoyote.

“Familia tano zilikuwa zinaishi hapa, vyumba vyote sita vimeungua kabisa. Tunaomba msaada kwa waathirika maana hawana walichobakiwa nacho,” amesema.

Nyumba ya wapangaji iliyopo Mtaa wa kanisani,kata ya Bomambuzi, Manispaa ga Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kuteketea kwa Moto. Picha na Yese Tunuka



Mwenyekiti wa Mtaa wa Kanisani, Kata ya Bomambuzi, Juma Mohamed Juma amesema alisikia kelele za wananchi na kukimbilia eneo la tukio kabla ya kuwataarifu Zimamoto.

“Wananchi pamoja na bodaboda walisaidia kutoa taarifa na kuwaelekeza Zimamoto hadi eneo la tukio,” amesema.

Mmoja wa wapangaji katika nyumba hiyo, Juma Salehe ambaye mfanyabiashara wa mbogamboga katika Soko la Manyema amesema amepoteza mali nyingi pamoja na Sh2.5 milioni alizokuwa ameandaa kwa ajili ya biashara.

“Televisheni, vitanda vya watoto, masofa, friji, kabati, nguo na fedha zote zimeungua. Naamini chanzo ni hitilafu ya umeme kwa sababu hakuna aliyekuwa anapika,” amesema.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na uchunguzi huku likiwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto majumbani.