Viongozi wa dini wataka wananchi kuliombea Taifa

Mbeya. Viongozi wa dini mkoani Mbeya wamewaomba wananchi kutumia vyema mwezi wa Ramadhan na Kwaresima kufanya toba, kuomba amani, huruma na msamaha kwa Mungu ili Taifa liendelee kuwa salama.

Pia, wamewataka wananchi kujinyenyekeza kwa Mungu na kulaani matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu, Oktoba 29 kutojirudia ili kutengeneza kizazi chenye maadili kwa jamii.

Akizungumza leo Februari 14, Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Msafiri Njalambaha amesema mwezi wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza wiki ijayo ni ibada inayoweza kubadili maisha ya mwanadamu, hivyo kila mmoja anapaswa kutii amri hiyo haswa kwa Waislamu.

Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Msafiri Njalambaha (katikati) akiongoza dua maalumu kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadan.



Amewatahadharisha wafanyabiashara kutotumia kipindi hicho kupandisha bei ya bidhaa sokoni, badala yake wajiweke karibu na Mungu kwa kufanya bei kuwa ya chini ili kusaidia mwananchi kufunga katika mazingira mazuri.

“Tuiombee nchi yetu amani kwani bila hili hatutafanya lolote, lakini tuombe huruma kwa Mungu, hizi ibada kutokea kwa pamoja ni mipango yake na kile kilichotokea Oktoba 29 iwapo ni kwa makosa yetu tusamehewe lisijirudie, tutubu sana” amesema Sheikh Njalambaha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu mkoani humo (Juwakita), Mwanne Said amewataka wazazi kutokuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili kwa vijana akiwaomba kutimiza wajibu wao.

“Vijana wajitambue na kumcha Mungu, watafute riziki za halali tudumishe amani yetu, lakini wazazi na walezi wasiwe chanzo kwa mmomonyoko wa maadili, kila mmoja atimize vyema wajibu kwa kipindi cha Ramadhan” amesema Mwanne.

Askofu wa Kanisa la Angelical Brotherhood Tanzania, Rabbi Mwakanani.



Naye Askofu wa Kanisa la Evangelical Brotherhood Tanzania, Rabbi Mwakanani amesema kila mmoja anapaswa kujitathimini, kutubu na kuomba msamaha kwa yaliyojitokeza Oktoba 29 wakati na baada ya uchaguzi.

“Kila mmoja atimize wajibu wake kuanzia jamii na mamlaka zote wakiwamo viongozi wa dini ambao ndio wenye jukumu la kuhamasisha amani, tuache masilahi binafsi na kuegemea upande mmoja, hii ibada iwe sehemu ya kutuunganisha pamoja” amesema.