Wananchi 1,123 Ifakara wapewa kadi za bima ya afya kwa wote

Ifakara. Halmashauri ya Mji Ifakara imeendelea na mpango wa kugawa kadi za bima ya afya kwa wananchi walioainishwa kwenye mpango huo mpaka sasa walioandikishwa na kupewa kadi ni 1,123 kati ya 4,161 wanaolengwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango huo leo, Jumamosi  Februari 14 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Pilly Kitwana amesema mpaka sasa kata 12 kati ya 19 zimeshafikiwa.

Kata hizo ni Ifakara, Lumemo, Michenga, Kibaoni, Lipangalala, Mlabani, Mbasa, viwanja sitini, Katindiuka, Signal, Kiberege na Kisawasawa.

Kitwana amesema kadi hizo zimetolewa kwa makundi ya wazee, wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, watu wenye mahitaji maalumu pamoja na kaya zenye hali duni ya kipato.

Aidha Kitwana amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa bima ya afya kwa wote  hatua iliyowaletea faraja wananchi wengi katika mji huo

“Gharama za bima ya afya kwa kundi hili zinalipiwa na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wote hususani makundi yenye uhitaji maalumu wanapata huduma bora za afya bila kikwazo cha fedha,” ameeleza Kitwana.

“Utekelezaji wa mpango huo umeleta tabasamu kwa wananchi, hususan wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu bila ya kuwa na bima ya afya.”

Mratibu wa Tasaf Ifakara Mji Brigita Haule, amesema bima hizo ni muhimu sana kwani zitawasaidia wananchi wanapopatwa na changamoto za kiafya kuhudumiwa bila vikwazo na kwamba  ugawaji wa kadi unaendelea katika kata zote 19 za Halmashauri ya Mji Ifakara.

Mmoja wa wanufaika wa bima hizo Safina Ninje, amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia kadi za  bima ya afya na kusema kuwa ni msaada mkubwa na unawapa uhakika wa matibabu.

Mpango huo unaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuinua ustawi wa wananchi.