Watu watatu waliohukumiwa kunyongwa kwa mauaji waachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufaa iliyoketi Mbeya, imewaachia huru watu watatu waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji.

Walioachiwa huru ni Masikitiko Lusambo, Huruma Mwasile na Aman Mswima ambao Juni 22,2023 walihukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya Shukuru Sandala.

Warufani hao na mtu mwingine (ambaye aliachiwa huru baada ya kukutwa hana hatia), walishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Mauaji hayo yalidaiwa kutokea Februari 9,2020 katika eneo la Mtakuja Mbalizi,  mkoani Mbeya, katika rufaa hiyo namba 761/2023 warufani hao walipinga hukumu.

Uamuzi uliowaachia huru warufani hao umetolewa Februari 13,2026 na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu nchini ambao ni Rehema Kerefu, Lucia Kairo na Deo Nangela.

Baada ya kupitia mwenendo, sababu za rufaa Mahakama ililibaini kuwa Mahakama Kuu ilikosea kisheria kwa kutegemea ushahidi wa kimazingira usiokidhi viwango vya kuthibitisha hatia bila shaka yoyote.

Majaji walieleza kuwa kulikuwa na tofauti kubwa kati ya maelezo ya shtaka na taarifa ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, hasa kuhusu tarehe ya tukio na majina ya marehemu.

Wameeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria, tofauti kama hizo zilipaswa kurekebishwa kupitia marekebisho ya shtaka, jambo ambalo halikufanyika.

Aidha, Mahakama ilibaini kuwa upande wa mashtaka haukuita mashahidi muhimu, akiwamo daktari aliyefanya uchunguzi mwili wa marehemu, wala kuwasilisha ripoti ya uchunguzi baada ya kifo kuthibitisha chanzo cha kifo.

Wameeleza vielelezo vilivyodaiwa kupatikana eneo la tukio, kama kisu na koti lenye madoa ya damu pamoja na ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali, pia havikuwasilishwa mahakamani.

Majaji walisisitiza kuwa katika kesi zinazotegemea ushahidi wa kimazingira, lazima ushahidi huo uunde mnyororo kamili usioacha nafasi ya shaka na katika kesi hiyo walibaini kuwa mnyororo huo haukuundwa ipasavyo.

Kutokana na upungufu huo, Mahakama iliridhika kuwa kesi ya upande wa mashtaka haikuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, hivyo, kuruhusu rufaa, kufuta hukumu ya kifo na kuamuru warufani waachiliwe huru mara moja isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.

“Baadhi ya mashahidi muhimu, nyaraka na vitu vilivyoorodheshwa wakati wa usikilizwaji wa awali, kisu na koti ambavyo vilidaiwa na shahidi wa sita vilipatikana eneo la tukio, havikuwasilishwa mahakamani na hakukuwa na maelezo yoyote yaliyotolewa na upande wa mashtaka kwa kutofanya hivyo,”

“Pia ni kumbukumbu kwamba, maelezo ya onyo ya washtakiwa wengine ingawa yaliorodheshwa wakati wa kesi, kukabidhiwa dhamana na usikilizwaji wa awali, hazikuoneshwa katika kesi hiyo ili kutoa mwanga zaidi kuhusu jambo hilo.

“Zaidi ya hayo, daktari aliyechunguza mwili wa marehemu na kuandaa ripoti ya uchunguzi wa kifo pia hakuitwa na ripoti ya uchunguzi wa kifo pia haikuoneshwa ili kubaini chanzo cha kifo. Tena hakukuwa na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka ikiwa shahidi huyo hangeweza kupatikana,” ameongeza Jaji.

Awali, ushahidi wa mashtaka uliotolewa Mahakama Kuu ulidai kuwa marehemu alikuwa akifanya kazi katika baa ya urafiki.

Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Furaha Moses, alidai kumwomba dereva bodaboda ampeleke nyumbani akitokea katika baa hiyo.

Alidai kuwa badala yake marehemu alielekezwa kumpeleka nyumbani kwa kutumia bodaboda hiyo na walipofika mnara wa mawasiliano walikutana na watu waliowasimamisha wakiomba usafiri.

Alidai marehemu aliwatambua kwa majina kuwa ni Haruna na Aman na kuahidi kurudi kuwachukua, ambapo alipelekwa nyumbani kwake na baadaye usiku alipata taarifa kuwa Shukuru ameuawa karibu na eneo hilo la mnara wa mawasiliano.

Shahidi wa pili, Mary Mwazyunga (mke wa shahidi wa kwanza), aliieleza Mahakama kuwa siku ya tukio mumewe alifikishwa nyumbani na Shukuru na baadaye walipokea taarifa za kifo chake.

Shahidi wa tatu ambaye ni kaka wa marehemu, Maiko Njebele, alithibitisha Mahakama kuwa siku ya tukio Shukuru alikuwa kazini na kuwa baadaye alipokea taarifa ya kutokurudi baada ya kumpeleka shahidi wa kwanza nyumbani kwake na kugundua baadaye kuwa ameuawa na alienda kutambua mwili wake hospitali.

Kwa upande wake shahidi wa tano, Ezekiel Mwaweza, alithibitisha mazingira ya mwisho ya marehemu kabla ya tukio  na kwamba alimruhusu ampeleke shahidi wa kwanza nyumbani kwa kutumia pikipiki yake.

Shahidi wa sita ambaye ni Ofisa Upelelezi wa Polisi, H 4910 DC Hassani, aliieleza Mahakama kuwa alifika eneo la tukio saa sita usiku akiwa na maofisa wengine wa polisi na kukuta mwili wa marehemu ukiwa na jeraha usoni.

Alidai walikuta pia kisu kilichovunjika na koti lenye madoa ya damu, kisha wakachukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitalini na akaandaa ramani ya mchoro wa eneo la tukio.

Mrufani wa kwanza, alidai kukamatwa Februari 10,2020 akiwa nyumbani kwake na kupelekwa Kituo cha Polisi Mbalizi na siku iliyofuata aliandika maelezo  akidaiwa kuhusika na wizi wa pikipiki.

Alidai baadaye Aprili 8,2020 walifikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji na kukana maelezo yake ya onyo akidai alilazimishwa kusaini tarehe aliyofikishwa mahakamani bila kujua yaliyomo.

Mrufani wa pili alidai kukamatwa Februari 10,2020 saa nane mchana katika klabu ha pombe huku mrufani wa tatu akidai kukamatwa Februari 13,2020 akiwa anatoka klabu ya pombe bila kuambiwa kosa lake ambapo warufani wote walikana kujuana na kuwa walikutana kwa mara ya kwanza Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakati alama za vidole zinakusanywa.

Katika rufaa iliyowaachia huru, warufani hao walikuwa na sababu mbili ambazo ni Jaji alifanya makosa katika kuwatia hatiani na kuwahukumu kwa kuzingatia ushahidi wa kimazingira ambao haukuwa wa kuaminika.

Sababu nyingine ni Jaji alikosea kuwatia hatiani na kuwahukumu huku kesi ya upande wa mashtaka ikiwa haijathibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote.