Waziri Mkuu aagiza mkandarasi aliyekula fedha za maji, akamatwe

NA MASHAKA MHANDO, Korogwe

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (RPC), ACP Almachius Mchunguzi, kumsaka na kumkamata mkandarasi aliyekimbia baada ya kulipwa Shilingi Milioni 934 kwa ajili ya ukarabati wa mradi wa maji katika mji wa Mombo, wilayani Korogwe.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo Leo February 14 mara baada ya kukagua mradi wa maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika wilaya nne za mkoa wa Tanga, ambapo ameeleza kukerwa na mkandarasi huyo aliyepokea fedha za umma na kutoweka bila kutekeleza mradi, huku wananchi wakiendelea kutaabika na ukosefu wa maji.

“Ameondoka na fedha wakati wananchi wanapata shida; haya ndiyo mambo yanayokera na kuchukiza. RPC, huyu mtu atafutwe popote alipo, akamatwe na awekwe ndani mpaka arejeshe fedha za umma. Sijateuliwa ili nipendwe, na sitakuwa na huruma na watu wanaohujumu miradi ya Serikali,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Mradi wa Miji 28 Kufikia Asilimia 75

Mapema, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, alimweleza Waziri Mkuu kuwa mradi wa maji wa Miji 28 unaogharimu Shilingi Bilioni 171 umefikia asilimia 74 ya utekelezaji wake. Mradi huo unatarajiwa kuwa ukombozi kwa wakazi wa wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza, na Pangani.

Waziri Aweso alibainisha kuwa mradi huo utazalisha lita milioni 52 za maji kwa siku, zitakazohudumia wananchi wapatao 860,000 katika vijiji 161. Alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo na kueleza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi, 2026.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa maelekezo ya haraka kwa wataalamu wa maji kuhakikisha wananchi wa Kijiji cha Tabora, Kata ya Mswaha (Korogwe Vijijini), ambao mradi unapita katika maeneo yao, wanapatiwa huduma ya maji mara moja ili nao wanufaike na matunda ya uwekezaji huo mkubwa.

Dkt. Mwigulu alihitimisha kwa kusema kuwa Serikali itaendelea kuwa na msimamo mkali dhidi ya mkandarasi yeyote atakayefanya kazi chini ya kiwango au kuiba fedha za miradi, akisisitiza kuwa thamani ya fedha lazima ionekane kwa wananchi.

Mapema asubuhi Waziri Mkuu akiwa wilayani Kilindi  ametoa onyo kali kwa wasimamizi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi, akisema atachukua hatua kali za kinidhamu na kisheria endapo itabainika kuwepo kwa ubadhirifu wa Shilingi Bilioni 2.6 zilizotolewa kwa ajili ya mradi huo.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la hospitali hiyo, ambapo licha ya kuridhishwa na ubora wa majengo yaliyokamilika, ameshitushwa na taarifa za kutoonekana kwa jengo la wodi ya mama na mtoto wakati fedha zake zilikwishatolewa na Serikali.

“Nimekuja kuweka jiwe la msingi baada ya kuridhishwa na viwango vya ujenzi wa majengo haya, lakini DED nimeambiwa fedha iliyokuja ilitakiwa ijenge majengo mengi zaidi ya haya. Nyinyi mmejenga majengo pungufu, fedha nyingine mmeipeleka wapi?” alihoji Waziri Mkuu.

Sakata la Saruji ya Mbeya na “Kichaka” cha Gharama.

Waziri Mkuu amefichua mchezo unaofanywa na baadhi ya watumishi wa kuhalalisha matumizi mabaya ya fedha kwa kununua vifaa vya ujenzi mbali na maeneo ya mradi ili kuongeza gharama za usafirishaji. Ameshitushwa na taarifa kuwa saruji ya ujenzi wa hospitali hiyo imenunuliwa mkoani Mbeya badala ya kutumia viwanda vya saruji vilivyopo jirani mkoani Tanga.

“Kuna mchezo unataka kuhalalishwa hapa wa kununua vifaa mbali; najua saruji mmenunua Mbeya. Takukuru fuatilieni kila kitu kwenye hiki kichaka cha gharama ili niweze kuchukua hatua kali. Hatuwezi kuwavumilia watu wanaoisababishia Serikali hasara kiasi hiki,” alisisitiza.

Mapema, John Mgalula Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi (DED), alikiri mbele ya Waziri Mkuu kuwa fedha zilipokelewa kwa ajili ya majengo tisa, lakini majengo ya kufulia na kutolea dawa hayajakamilika kutokana na kile alichodai kuwa ni kuongezeka kwa gharama za kusafirisha vifaa.

Mgogoro wa mpaka kati ya Simanjiro na Kilindi

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amechukua hatua za haraka kutatua mgogoro wa mpaka kati ya wilaya za Simanjiro (Manyara) na Kilindi (Tanga), ambao umedumu kwa muda mrefu na kusababisha mivutano kati ya wakulima na wafugaji.

Waziri Mkuu ametangaza kuunda Kamati ya Mawaziri wa Kisekta itakayojumuisha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii, pamoja na TAMISEMI ili kumaliza kabisa mgogoro huo na kurejesha amani katika maeneo ya mipakani.

Kikao hicho kitakutana mkoani Tanga February 16 kabla Waziri Mkuu hajaondoka mkoani hapa kuelekea mkoani kilimanjaro