Geita. Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kasala ameshauri utaratibu wa utoaji wa Bima ya Afya kwa Wote nchini uzingatie haki na upendo, bila kuweka madaraja yanayosababisha utengano baina ya wanajamii.
Ameongeza kuwa ugunduzi wa kitabibu unaofanyika duniani, unalenga kuwanufaisha watu wote bila kujali madaraja ya vipato vyao ambapo amesema anatiwa shaka na tafsiri inayotolewa kuhusu bima hiyo ikiwa inazingatia haki za watu wote kupata matibabu bila kujali daraja la kiuchumi.
“Hivi kama bima ya afya kwa wote itawekwa katika vigezo kwa kuangalia fedha walizonazo watu mfukoni, huo uwote uko wapi?
“Kama tunasema Malaria inaua wote, lakini matibabu yake tunayatoa kwa kuangalia nani ana fedha nyingi zaidi, haina tena maana kwa wote,” amesema Askofu Kasala.
Askofu wa jimbo Katoliki la Geita Flavian Kasala, akizungumza katika misa iliyoambatana na kufungwa kwa huduma ya matibabu bure katika Kanisa kuu Jimbo katoliki la Geita.
Askofu Kasala ametoa kauli hiyo leo Februari 15, 2026 katika misa iliyoambatana na kufungwa kwa huduma ya matibabu bure, iliyoanza kutolewa jimboni humo ikitekelezwa na wataalamu wa afya ambao ni waumini wa kanisa hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mmoja wa wahudumu wa afya Jimbo Katoliki la Geita, Dk Sadoki Mathias kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita, amebainisha kuwa kila mwaka wamekuwa na utaratibu wa kumshukuru Mungu kwa kutoa huduma za vipimo na matibabu bure kwa watu wote bila kujali itikadi zao.
Kwa mwaka huu, huduma zilizokuwa zikitolewa ni pamoja na vipimo na matibabu kwa magonjwa yasiyoambukizwa kama kisukari, selimundu, huduma za kibingwa kwa watoto, tohara kwa wanaume, pua, koo na sikio, kinywa na meno, macho sambamba na uchangiaji.
Dk Sadoki Mathias, kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita, akizungumza wakati wa kuhitimisha huduma za vipimo na matibabu bure, katika huduma iliyofanyika Kanisa kuu Jimbo katoliki la Geita.
Wananchi zaidi ya 300 wamenufaika na huduma zilizotolewa ambapo watu 169 wamepatiwa huduma ya vipimo, watoto 11 wa kiume wamefanyiwa tohara, huduma ya pua na koo zimetolewa kwa watu 28.
Vilevile, huduma za macho zimetolewa kwa wananchi 48 ambapo wameiomba Serikali kuongeza nguvu katika huduma hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu wanaosumbuliwa na macho.
Akizungumza baada ya kuhitimisha huduma hiyo, Dk Joseph Charles ameshauri wazazi na jamii kwa ujumla kuwa na mazoea ya kupima kila wakati ili kukabiliana na matatizo ya magonjwa yasiyoambukizwa.
Katika Mkoa wa Geita, Serikali imeanza utekelezaji wa mfumo wa Bima ya Afya kwa wote nchini huku kaya 11,276 zikitambuliwa na kuanza kusajiliwa tayari kuanza kunufaika kwa awamu ya kwanza mkoani humo kwa watu walio na kipato cha chini kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf).