Dar es Salaam. Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimeeleza kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa miundombinu na vifaa vya kufundishia ikiwamo meli ya kufanyia mazoezi kwa vitendo kwa mabaharia wanafunzi.
Kimesema kimekuwa kikitumia simulator (kifaa kinachofanana na meli) katika mafunzo kwa vitendo, hivyo kuiomba Serikali iwasaidie kipate meli ya mazoezi kwa vitendo, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi zaidi kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyotembelea chuoni hapo leo Februari 15, 2026, Mkuu wa Chuo, Profesa Tumaini Gurumo amesema wana upungufu wa miundombinu ya kufundishia na madarasa.
“Tuna changamoto ya meli ya mafunzo, tukifanikiwa kuondokana na changamoto hii, tunatarajia vijana wetu wengi watapata fursa za ajira,” amesema Profesa Gurumo.
Kuhusu madarasa, amesema: “Hapa chuo kilipo, kipo tangu miaka ya 1970, hivi tumepata eneo Kimbiji ambako tunatarajia hadi 2027, sehemu kubwa ya chuo iwe imehamia huko huku upanuzi kwenye maeneo yetu ya Mkuranga na Lindi ukiendelea katika hatua mbalimbali.
Amesema chuo hicho ambacho ni moja ya vyuo vikubwa vya Bahari Afrika, kinatoa mafunzo kwa viwango cha kimataifa na wahitimu wake wana uwezo wa kufanya kazi katika nchi yoyote.
Mkuu huyo wa chuo amesema ubora wa elimu wanayoitoa kama Serikali itasaidia chuo kipate meli ya mafunzo kwa vitendo, Tanzania itapiga hatua kubwa zaidi katika sekta ya mabaharia.
Wakitoa mapendekezo kwa Wizara ya Uchukuzi, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, walishauri kwenye bajeti ya Wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27 waiangalie DMI kwa jicho la huruma.
Walisema kufundishwa ubaharia kwenye makaratasi ni sawa na sifuri, wakiitaka wizara itoke huko na iweke historia ya kununua meli ya kufanyia mazoezi kwa vitendo kwenye chuo hicho ili wanafunzi mabaharia wajifunze kwa uhalisia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abubakari Asenga ameshauri Serikali izingatie hoja za wajumbe wa kamati hiyo ya kutakiwa iongeze uwekezaji kwenye chuo hicho.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa wizara hiyo, David Kihenzile amesema wamepokea ushauri na kusisitiza kwamba katika kipindi hiki umuhimu wa chuo hicho unaonekana zaidi.
“Tumesikiliza kwa makini hoja ya kutaka Serikali iongeze uwekezaji kwenye chuo hiki, tumeipokea japo tulishaanza na kwa kuwa ninyi (wajumbe wa kamati) mmeliona pia, basi tutalifanyia kazi, japo ukiangalia tulipotoka na tulipo huwezi kulinganisha,” amesema.
Amesema kama nchi inahitaji kuwa na wataalamu wa kutosha huku akibainisha kwamba kwa miaka mitano ya nyuma, udahili wa wanafunzi katika chuo hicho umeongezeka zaidi.