Dar es Salaam. Kushamiri kwa bandari bubu nchini, kumeiamsha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kutoa maagizo kwa Serikali kuweka mkakati wa kudhibiti bandari hizo, kwani ndio lango la uingizwaji wa dawa za kulevya.
Mbali na dawa kulevya, kamati hiyo imesema bandari bubu ni uchochoro unaotumika kupitisha bidhaa zisizohitajika nchini.
Kauli hiyo inakuja wakati ambapo aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Suleiman Jafo Machi 20, 2025 kwenye mkutano na wenye viwanda nchini alisema kuwa, bandari bubu ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato (TRA) kukabiliana nayo.
Leo Februari 15, 2026 akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso amesema bandari bubu ni eneo linalotumika kupitisha bidhaa haramu.
“Njia pekee ambayo dawa za kulevya hupitishwa ni majini hivyo tumeishauri Serikali kuweka mkakati wa kudhibiti bandari bubu.
“Bandari bubu inaweza kuwa jambo hatari sana kwenye maeneo yetu, tumeishauri pia Tasac kuangalia mifumo ya kuwawezesha kutoa elimu ya mafunzo, kwani lazima watumishi wawe na vifaa wakati wa utoaji wa elimu,” amesema.
Kakoso amesema changamoto nyingine waliyobaini ndani ya Tasac ni ukosefu wa vifaa akisisitiza shirika hilo linahitaji uwekezaji mkubwa wa vifaa vya uokozi katika ukanda wa bahari, ziwa Tanganyika, Nyasa na Ziwa Victoria.
“Tumeishauri Serikali kuongeza bajeti, kuweka mifumo ambayo itasaidia kupunguza ajali zinazojitokeza mara kwa mara, tumeielekeza palipo na vikwazo tuelezwe kama Bunge tuchukue nafasi ya kusimamia, kazi ya Bunge ni kusimamia Serikali na kuishauri.
Kakoso amesema Tasac kuna vikwazo vya kisheria hivyo wameielekeza Serikali waharakishe mchakato wa kupeleka sheria bungeni, zifanyiwe marekebisho na wao wapo tayari kuwasaidia, ili taasisi isimame vizuri.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum amesema yapo baadhi ya maeneo ambayo hakuna miundombinu ya bandari, udhibiti wa Serikali lakini zipo shughuli zinafanyika na ndizo zinaonekana kuwa bandari bubu.
“Mwaka 2022/2023 hadi 2023/2024 tumefanya jitihada kubwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kurasimisha bandari bubu 20 katika maziwa na bahari, lakini pamoja na kurasimisha bado zipo bandari bubu nyingi,” amesema.
Amesema zipo juhudi zinafanyika kuhakikisha maeneo yote yenye bandari bubu yanadhibitiwa ili kutoingizwa magendo nchini.
“Tunashirikiana na halmashauri na maofisa uvuvi wanatoa elimu kwa wavuvi kutumia maeneo rasmi na sio kwenda kwenye bandari kavu na tutaendelea na maeneo mengine,” amesema.
Sheria ya Bandari Na. 17 ya mwaka 2004, kifungu cha 5 kinaipa TPA mamlaka ya kuanzisha, kuendesha na kusimamia bandari zote zilizopo Bahari ya Hindi na maziwa nchini.
Sheria hii pia inasimamia maendeleo ya miundombinu ya bandari na kuhakikisha huduma bora kwa wateja, inazuia uanzishaji wa bandari zisizo rasmi kwa kufafanua taratibu maalumu za kufuatwa kabla ya kuanzisha bandari yoyote na kuhakikisha shughuli za bandari zinasimamiwa kikamilifu na ΤΡΑ.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi mwaka jana umebaini katika Mkoa wa Dar es Salaam, baadhi ya bidhaa za magendo hupitia kwenye bandari bubu zilizopo Mbweni Kigamboni na Bagamoyo mkoani Pwani.
Licha ya Mbweni na Kunduchi zilizokuwa miongoni mwa bandari bubu maarufu kurasimishwa, bado wanaojishughulisha na biashara ya magendo wametafuta maeneo mengine jirani kuendelea na kazi hiyo isivyo halali.
Mkoani Lindi, maeneo yanayotumiwa kupitisha bidhaa za magendo ni Somanga na Safina, yaliyopo Kilwa Kivinje, yanayotumika kutokana na mazingira yake ya mikoko mingi.