Kariakoo Dabi ya Machi mosi kupigwa ‘Gwantanamo Bay’

MECHI ya watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba maarufu Kariakoo Dabi iliyopangwa kufanyika Machi 1, 2026, itachezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ambao ni wenyeji wa mechi hiyo ikiwa ni ya mzunguko wa kwanza katika Ligi Kuu Bara.

Kamwe ametoa kauli hiyo muda mchache baada ya Yanga kuichapa JS Kabylie mabao 3-0 katika mechi ya mwisho hatua ya makundi, hata hivyo, timu hiyo imeshindwa kufuzu robo fainali ikimaliza nafasi ya tatu na pointi nane, nyuma ya vinara Al Ahly (10) na AS FAR Rabat (9). JS Kabylie imekamata mkia na pointi tatu.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Kamwe ameandika: “Mchezo wetu wa Ligi Kuu Machi 1, 2026 dhidi ya Simba SC, ‘Kariakoo Derby’ utapigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex saa 2:15 Usiku. Karibuni sana.”

Kwa mujibu wa ratiba iliyofanyiwa maboresho na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kisha kutangazwa Novemba 17, 2025, mechi hiyo namba 54, ilipangwa kufanyika saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, lakini sasa wenyeji wameipeleka Zanzibar.


Ikumbukwe kuwa, mechi hiyo inayobeba hisia za mashabiki wengi, katika ratiba ya awali iliyotangazwa Agosti 29, 2025, ilionyesha ingechezwa Desemba 13, 2025, lakini ikasogezwa mbele hadi Machi 1, 2026 kupisha maandalizi ya Taifa Stars iliyoshiriki AFCON 2025 nchini Morocco, fainali zilizoanza Desemba 22, 2025 hadi Januari 18, 2026 ambapo Senegal ilitwaa ubingwa kwa kuwachapa wenyeji Morocco kwa bao 1-0.

Yanga imefikia uamuzi wa kuutumia uwanja huo kwa mechi hiyo kama ilivyofanya msimu uliopita ilipocheza dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi ya mwisho kuhitimisha msimu.

Mbali na hilo, pia msimu huu Yanga imeutumia Uwanja wa New Amaan Complex kwa mechi zake za nyumbani katika kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika, ikifanikiwa kuwa na rekodi nzuri ya kutopoteza ikishinda mbili dhidi ya AS FAR Rabat (1-0) na JS Kabylie (3-0), huku ikitoka sare ya 1-1 na Al Ahly.

Katika mashindano ya ndani, msimu huu Yanga mechi za nyumbani imeutumia Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.