Tabora. Baadhi wachimbaji wadogo wa madini wamemuomba Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Kenani Kihongosi kuingilia kati mgogoro baina yao na mwekezaji.
Chimbuko la mgogoro huo umetokana na mwekezaji huyo raia wa kigeni anayetaka kuendeleza eneo hilo, kuwapa miezi mitatu kuhamisha mali zao, muda walilodai hautoshelezi.
Hata hivyo, Kihongosi amewatoa hofu akimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo kwenda wiki ijayo kusikiliza pande zote ili kupata ufumbuzi.
Wachimbaji hao walitoa malalamiko hayo kupitia mabango walioandika ujumbe huo leo Jumapili Februari 15,2026 wakati Kihongosi alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa shule ya awali ya Iborogero wilayani Igunga.
Mkazi wa eneo hilo, Issa Miraji amesema wamekuwa wakiendesha shughuli za uchimbaji muda mrefu na kuchangia uchumi wa Igunga, lakini ghafla wanashangaa mwekezaji amekabidhiwa eneo hilo na wao wanatakiwa kuhama.
Wananchi na baadhi ya viongozi wa chama na serikali wakisikiliza maelekezo ya Katibu wa Nec,Itikadi,Uenezi na Mafunzo Kenani Kihongosi katika mradi wa shule mpya ndani ya Shule ya Msingi Iborogero
“Miezi mitatu haitoshelezi michache, ikilinganisha na mali za watu walizoziweka hapa katika mgodi huu,” amesema Miraji akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wenzake.
Miraji amefafanua kuwa ili mtu ahamishwe lazima ajue anapelekwa wapi na ataenda kufanya nini baada ya hapo, miezi mitatu haitoshelezi kwa ajili kujipanga.
“Sisi ni watu watulivu sana na tunapenda maendeleo ya nchi yetu, lakini sio kwa kuumizwa hivyo, halafu sisi hatuna tatizo kama mwekezaji anaweka mazingira mazuri kwa wachimbaji,” amesema Miraji.
Baada ya malalamiko hayo, Kihongosi alianza kwa kuwatoa hofu akisema pamoja na majukumu mengine lakini CCM ina kazi ya kusikiliza na kutatua kero za Watanzania, hivyo wasiwe na wasiwasi.
“Mkuu wa wilaya, nakuagiza Alhamisi ya wiki inayoanza hakikisha unakwenda kwenye hayo machimbo na uwasikilize changamoto zao. Maana wakati nazungumza hapa naona mabango hivyo ni dhahiri wana changamoto,” amesema Kihongosi.
Kihongosi amesema uwekezaji ni kitu bora lakini kuwepo kwa utaratibu mzuri, hivyo wachimbaji wa Iborogero wawe na amani kwa sababu Serikali italifanyika kazi suala hilo ili kila mmoja apate haki yake.
Kihongosi ameanza ziara ya siku tatu mkoani Tabora ambapo atatembelea na kuzungumza na wananchi wa Igunga, Nzega na Urambo kisha kuelekea Kigoma.
Akiwa Igunga amekagua miradi ya maendeleo ikiwemo shule na mradi wa ujenzi wa jengo la biashara la chama hicho lenye thamani ya Sh143 milioni.
Pia, katika ziara hiyo Kihongosi amekagua kituo cha kupokea, kupooza na kusambaza umeme cha Ziba na ujenzi wa shule mpya ndani ya shule ya msingi Iborogero.