Tabora. Ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege, kinachojengwa katika kata ya Mapambano, manispaa ya Tabora, umefikia asilimia 95.
Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha nguzo 120 kwa siku pindi ujenzi wake utakapokamilika.
Akizungumza Februari 14, 2026 baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amemuelekeza mkandarasi kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu.
Amesema mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho unatekelezwa na kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ya Tanzania Concrete Poles Manufacturing Company Limited (TCPM), lengo likiwa ni kutengeneza nguzo za zege ambazo zitakua na ubora wa hali ya juu na kwamba nguzo hizo zinadumu kwa muda mrefu zaidi ikilinganishwa na zile za magogo.
“Mradi huu unatekelezwa kwa makusudi kabisa kuhakikisha tunatatua changamoto ya kubadilisha nguzo mara kwa mara kutokana na changamoto hususani za kuoza, kwa hiyo rai yangu kwako mkandarasi ni kuhakikisha ubora wa Nguzo hiz uwe unaokusudiwa”amesema
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, akizungumza wakati anakagua mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza Nguzo za Zege katika kata ya Mapambano manispaa ya Tabora.
Amemuagiza mkandarasi kwamba asifanye kazi hiyo kwa haraka ili mradi amalize haraka, aifurahishe serikali alafu akajikuta anatengeneza chini ya kiwango, jambo ambalo litakuwa hatari kwa usalama wa watu kwa sababu nguzo hizo zitabeba waya zenye moto, hivyo ubora ni jambo la kipaumbele muhimu.
“Sasa kwa sababu umeniambia, wiki moja mbele kutoka sasa utakua umekamilisha mradi, uhakikishe unakuwa kwenye kiwango bora, usilazimishe tu kutukabidhi kazi ili tuone umemaliza alafu ikawa shida hapa kwenye viwango,” amesisitiza.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema mradi huo mpaka sasa unaendelea vizuri kwani umefikia asilimia 20 na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha nguzo 120 kwa siku, jambo ambalo litasaidia kuzalisha nguzo nyingi kwa kipindi kifupi.
“Kiwanda hiki kinakwenda kuwa mkombozi wa upatikanaji wa nguzo bora na za kisasa ambazo zinadumu, pia, jambo kubwa tu sasa ni kukamilisha ujenzi huu kwa ubora wa hali ya juu ili lengo la serikali liweze kufikiwa,” amesema.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi (wa Tatu kutoka Kulia) akizungumza wakati anakagua mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza Nguzo za Zege katika kata ya Mapambano manispaa ya Tabora.
Meneja wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege Tabora, David Myumbilwa amesema kwa sasa mradi utakwenda haraka na utakamilika mara moja kwa kuwa vifaa vyote vimeshafika eneo la kazi na kazi zilizobaki ni chache na kwamba kwa sasa hakuna changamoto yoyote itakayokwamisha mradi huo.
“Tuko imara, hapo awali tulipata changamoto ya kuchelewa kwa baadhi ya vifaa na hii ni kutokana na vifaa hivyo kupatikana nje ya nchi, ndio sababu ya kuchelewa kwa baadhi ya vifaa lakini sasa kila ambacho hakikuwepo sasa kipo, tuko sawa kwa kazi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella amesema mradi huo ni fursa kwa wakazi wa Tabora kwani makundi hasa ya vijana watapata ajira na uchumi utakua kwa sababu uhitaji wa mahitaji maalumu utakuwa mkubwa.
Ameahidi kwa kushirikiana na wakazi wa Tabora kuilinda na kuitunza miundombinu ya kiwanda hicho ili kidumu na kuleta tija zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya watu wa Tabora.
“Kiwanda hiki kwa wakazi wa Tabora ni fursa kubwa, hivyo tunafurahi zaidi lakini tutailinda na kuitunza ili iendelee kuwa na tija kwa wana Tabora,” amesema.