Mafaili ya Epstein yanavyobeba hatima ya jela kwa wanasiasa, matajiri – 5

Familia ya Kifalme ya Uingereza ni taasisi yenye nguvu kubwa, kuliko yoyote ulimwenguni.

Inaendesha ya dola ya United Kingodom (UK) na nchi nyingine 14. Nchi hizo ni Australia, Canada, Bahamas, Belize, Grenada, Jamaica, New Zealand, Papua New Guinea  Saint Kitts na Nevis, Saint Lucia, Saint Vincent na Grenadines.

Visiwa vya Solomon, Tuvalu, vilevile Antigua na Barbuda.

Koo ya kifalme ya Uingereza, ndiyo ambayo hutoa watawala (wakuu wa nchi) hizo. Maana yake, wanachama wa familia ya kifalme ya Uingereza, hulelewa na kukuzwa kiuongozi. Hulindwa na kupewa daraja kubwa kijamii kwa sababu ni viongozi kidola na kitamaduni.

Tatizo la mwanachama yeyote linakuwa ni la familia nzima. Aibu ya yeyote kwenye ukoo, inahusu ukoo mzima. Hivyo, Mwanamfalme Andrew Mountbatten-Windsor “Prince Andrew”, kutajwa kwenye Mafaili ya Epstein, inagusa ukoo mzima wa kifalme. Kashfa ya vitendo vya Andrew ni kashfa ya familia.

Andrew, ni mtoto wa tatu katika watoto wanne wa Malkia Elizabeth II. Kwa wanaume Andrew ni wa pili. Mtoto wa kwanza kuzaliwa ni Mfalme Charles III. Wakati Andrew anazaliwa, alikuwa anashika nafasi ya pili katika mnyororo wa kutawazwa kuwa mfalme wa UK, yaani nyuma ya Charles III. Maana yake, Charles III angepoteza sifa kabla hajapata mtoto, pengine sasa hivi Andrew angekuwa ndiye Mfalme wa UK na nchi nyingine 14.

Kwa nafasi ya Mfalme wa UK, Andrew angekuwa ndiye mkuu wa nchi 56 za Jumuiya ya Madola, zilizopo mabara yote, Afrika, Asia, Amerika Kusini, Kaskazini hadi nchi za visiwa kwenye Bahari ya Pacific. Ni kuonesha kuwa vitendo vya Andrew havipaswi kutazamwa kama dhambi za mtenda dhambi, bali uasi wa mpakwa mafuta ya uongozi wa kidunia.

Kwa utamaduni wa ufalme wa Uingereza, jina la Andrew halitajwi bila kutamka “Your Royal Highness”, yaani:“Utukufu Wako wa Kifalme.”

 Mtu huyo wa hadhi hiyo, ndiye ambaye mwanamke mtetezi wa walioathiriwa kingono na Epstein, Virginia Giuffre, alilalamika kubakwa naye mfululizo alipokuwa na umri wa miaka 17.

Virginia alisimulia kuwa baada ya kusafirishwa hadi London, UK, kwa maelekezo ya Epstein, alimbiwa afanye na Andrew, kila alichokuwa anafanya na Epstein. Mwongozo huo Virginia alipewa na Ghislaine Maxwell. Kukumbusha, Ghislaine alikuwa mpenzi na mshirika mkuu wa uhalifu wa kingono wa Epstein. Ghislaine yupo jela kwa sasa.

Kwa kushiriki mapenzi na kumfanyia masaji Andrew, Virginia alilipwa na Epstein Dola 15,000 wakati huo. Kikokotoo cha mfumuko wa bei, kinaonesha kuwa Dola 15,000 ya mwaka 2001, thamani yake ni sawa na Dola 27,452.46, ambazo kwa sarafu ya Tanzania kwa sasa ni Sh71.5 milioni.

Alipokamilisha kila alichotakiwa kufanya na Andrew, Virginia alirejea Marekani. Mwaka 2002, Virginia alisafirishwa kwenda Thailand, kujiunga na Shule ya Kimataifa ya Mafunzo ya Masaji, iliyopo Jiji la Chiang Mai. Akiwa Thailand, Virginia alikutana na mwalimu wa sanaa za mapigano (martial arts), raia wa Australia, Robert Giuffre.

Virginia na Robert walianza uhusiano wa kimapenzi, kisha walikwenda Australia. Kabla ya kuondoka Thailand kwenda Australia, Virginia alimpigia simu Epstein na kumweleza kuwa asingerejea tena Marekani kuendelea na mipango yao. Alimjulisha pia Ghislaine, ambaye ndiye aliratibu safari yake ya masomo Thailand.

Kisha, Virginia na Robert, walianza maisha ya ndoa yenye ukimya Australia, wakijikita na malezi ya watoto wao wadogo. Mwaka 2007, Virginia alianza kuwasiliana na mamlaka kuhusu vitendo vya Epstein. Hiyo ilikuwa baada ya Idara ya Polisi Palm Beach, kuanza kufanya upelelezi kwenye kasri la Epstein, vilevile Idara ya Intelijensia Marekani (FBI), ilikuwa ikifuatilia kwa ukaribu.

Ilikuwa hivi; Machi 2005, msichana mwenye umri wa miaka 14, aliripoti malalamiko yake ya kubakwa na Epstein kwenye Idara ya Polisi Palm Beach. Kwa mujibu wa msichana huo, ubakaji ulifanyika ndani ya kasri la Epstein, lililopo Palm Beach.

 Msichana huyo alilalamika kuwa alishawishiwa na mwanafunzi mwenzake kwenda kumfanyia masaji Epstein na angelipwa kiasi kizuri cha pesa.

Msichana huyo alieleza kuwa, alipoingia kwenye kasri la Epstein kumfanyia masaji, bilionea huyo alimfanyia mashambulizi ya kingono na kumbaka. Ilipofika Oktoba 2005, polisi walikuwa wameshapokea kesi nyingi za wasichana, mshatakiwa akiwa mmoja; Epstein.

Kilichoongeza msukumo wa kufanya uchunguzi ni kuwa aina yao ya malalamiko ya vitendo walivyofanyiwa, ilifanana. Wote walishawishiwa kwenda kumfanyia masaji Epstein, walipofika ndani, walilazimishwa kufanya ngono. Na kwa kuwa walikuwa mabinti wadogo, waliishia kubakwa.

Kufikia hapo, polisi hawakuwa na ajizi, zaidi ya kutoa hati ya upekuzi kwenye kasri la Epstein. Palm Beach. Katika upekuzi huo kwenye nyumba ya Epstein, walikuta chombo cha kuhifadhia taka, kilichokuwa namba za simu za watu mbalimbali. Namba nyingi zilikuwa za waathirika wa vitendo vya Epstein.

Kila mwenye namba ya simu kwenye karatasi zilizokutwa nyumbani kwa Epstein, alitafutwa. Epstein na Ghislaine kwa kutambua Virginia alikuwa na ushahidi muhimu dhidi yao, walimtafuta na kumuuliza kama alikuwa amezungumza na polisi au mamlaka nyingine yoyote ya kiusalama. Epstein na Ghislaine hawakujua kuwa hilo lilikuwa kosa upande wao. FBI walikuwa wakifuatilia, kwa hiyo waliweza kunasa mazungumzo ya Epstein, Ghislaine na Virginia.

Muda mfupi baada ya Epstein na Ghislaine kumtafuta Virginia, mwanamke huyo alipokea simu kutoka Jengo la J. Edgar Hoover, yalipo makao makuu wa FBI, Washington DC. Maofisa wa intelijensia kutoka FBI, walitaka ushirikiano wa Virginia, ambaye mwanzoni aliogopa. Maana alishaonywa kuwa kwenda kinyume na Epstein, hatima yake ni kutekwa au kuuawa.

Maofisa wa FBI walimweleza Virginia kuwa tayari walikuwa na taarifa kwamba yeye alikuwa mwathirika wa vitendo vya Epstein. Virginia hakutaka kuzungumza kwa kirefu. Alihofia maisha yake. Miezi sita baadaye, Idara ya Polisi Australia, walimtafuta Virginia na kuzungumza naye ana kwa ana. Hapo ndipo Virginia aliweza kufunguka inavyotakiwa.

Mwaka 2006, FBI kabla ya kuwasiliana na Virginia, Idara ya Polisi Palm Beach, walikuwa tayari wamekusanya ushahidi kuhusu Epstein. Walisaini viapo vya walalamikaji (baadhi ya waathirika) na mashahidi wengine, kisha walimfungulia Epstein mashitaka ya kufanya mapenzi na watoto wadogo kinyume na sheria.

Epstein alichukua wanasheria wakubwa na wenye nguvu Marekani kwa ajili ya kumtetea. Wanasheria hao ni pamoja na Alan Dershowitz, Jack Goldberger, Ken Starr, na Jay Lefkowitz. Ni hapo Mkuu wa Idara ya Polisi Palm Beach, Michael Reiter, alipata taarifa ya michezo kufanyika kwenye mashitaka, hasa baada ya kubaini shauri lingesimamiwa na Wakili Mkuu wa Jimbo la Florida, Barry Krischer.

Mei mosi, 2006, Reiter alimtaka Krischer ajiondoe kwenye kesi ya Epstein kwa sababu asingetenda haki. Krischer alikataa kujitoa. Uamuzi wa Reiter ukawa kuchukua ushahidi wote waliokusanya kwa ajili ya mashitaka dhidi ya Epstein, akaupeleka FBI.