KAIMU Kocha Mkuu wa TMA ya jijini Arusha, Omary Matwiko ‘Tico Tico’, amesema tangu winga mpya, Japhet Vedastus Makarai, ajiunge na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026, ameleta mageuzi makubwa kwenye eneo lote la ushambuliaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tico Tico, amesema tangu nyota huyo amejiunga na timu hiyo tayari mabadiliko makubwa yameanza kuonekana kwa uharaka katika eneo la ushambuliaji, huku ushindani wa nafasi ukiongezeka pia jambo ambalo ni nzuri kwao.
“Kati ya wachezaji 13, tuliowasajili dirisha dogo ni Makarai aliyeingia kwa haraka katika kikosi cha kwanza kwa sababu anaijua vyema timu, ingawa wengine wanaendelea kuzoeana taratibu kutokana na mbinu ninazowafundisha,” amesema Tico Tico.
Nyota huyo aliyeifungia African Sports mabao matatu msimu huu, amerejea tena katika kikosi hicho ili kukiongezea nguvu kwenye eneo la ushambuliaji, huku akiwahi kuzichezea pia klabu mbalimbali za Kagera Sugar, Gwambina na Coastal Union.
Matwiko anayefananishwa na mshambuliaji wa zamani wa Msumbiji, Manuel Jose Luis Bucuane ‘Tico Tico’, anakiongoza kikosi hicho kwa muda, baada ya mabosi wa timu hiyo kuvunja benchi lote la ufundi lililokuwa chini ya Kocha Mkuu, Habibu Kondo.
Kabla ya mechi ya jana dhidi ya B19 FC iliyokuwa inachezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, TMA iko nafasi ya 11 na pointi 17, baada ya kushinda minne, sare mitano na kupoteza minane, ikifunga mabao 10 na kuruhusu 14.