UNAMKUMBUKA kocha wa zamani wa Yanga, Hans Pluijm? Sasa Mholanzi huyo anayeishi Ghana amevunja ukimya kwa kuichambua Simba kwa namna alivyoifuatilia katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na kutoa sababu kwa nini haijaingia robo fainali ya michuano hiyo licha ya kuwa na wachezaji bora.
Pluijm aliyewahi kuzinoa pia Azam FC na Singida United, amesema alivyotazama kiwango cha mchezaji mmoja mmoja wa Simba, asilimia kubwaya mastaa wenye uwezo wa juu ni wale waliyjiunga na timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo na anaamini wangekuwepo tangu maandalizi ya msimu mpya, klabu hiyo ingeenda robo fainali.
“Simba ina wachezaji wazuri ila wengi wao wameingia usajili wa dirisha dogo, timu imeanza kufanya vizuri mechi za mwishoni, jambo la msingi ni makocha, viongozi na wachezaji wenyewe kukubali uhalisia wa sasa kwa faida ya kufanya vizuri kipindi kijacho,” amesema Pluijm na kuongeza;
“Kama wachezaji waliopo Simba wataendelea kuwepo na wakawa na muendelezo wa kiwango, msimu unaokuja itakuwa moja ya timu tishio katika michuano ya CAF, kocha atakuwa amepata muda mzuri wa kutengeneza kombinesheni ya wachezaji kucheza kitimu zaidi na kuusoma uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.”
Amesema ukitaja timu zenye ushindani katika michuano ya CAF, Simba ni mojawapo na kipindi inachopitia kiwe mwanzo wa kujiimalisha zaidi na kurejea kwa nguvu nyingine.
“Yanga inayofanya vizuri kwa sasa ukiangalia asilimia kubwa ya wachezaji wamekaa pamoja kwa muda mrefu, hilo linawasaidia kujuana vizuri,” amesema.