ONGEA NA AUNT BETTIE: Mume wangu ‘amekata pumzi’ kitandani baada ya ndoa

Sijui alikuwa anajiunga na maungaunga ya kuongeza nguvu za kiume ama vipi. Maana alivyokuwa tulipokuwa wapenzi na sasa ni tofauti. Anti hata sijui nikuambie nini, ningejua mume wangu hajiwezi kitandani hivi, nisingefunga ndoa naye maana nahisi nitakuwa msaliti kwa sababu hana anachonifanyia zaidi ya kujipigisha makelele.

Ila tulivyokuwa wapenzi tunakutana mara moja moja alikuwa shababi hasa nikasema mume si ndiyo huyu, ila yanayonikuta sasa ninahitaji ushauri, maana sijioni nikitoboa.

Kwanza pole. Ila naomba uelewe mabadiliko ya mumeo baada ya ndoa ni jambo linalowatokea baadhi ya watu, hasa pale mtazamo wa kibinafsi, changamoto za afya, au mawazo kutokana na kuongezeka kwa majukumu ya familia kunapoanza kuathiri hisia zake. Kwa sababu sijampima nakujibu kutokana na ulichonieleza mumeo anaweza kuwa na changamoto ya kiafya au ya kisaikolojia ambayo inakwamisha ufanisi wake wa kitandani.

Hii haimaanishi hawezi kuwa sawa, bali ni ishara kuna kitu hakipo sawa.

Ili awe sawa kwanza acha kumwambia maneno ya kukera kuhusu hali yake ya sasa au akikuhitaji faragha kuanza kusema anakusumbua kwa sababu hakuna atakachokufanyia, ukifanya hivi utazidi kumpoteza kabisa.

Badala yake, unaweza kumueleza hali hiyo kwa njia ya upole na inayomaanisha kujenga kwa pamoja na itapendeza zaidi ukijiingiza kwenye hilo tatizo.

Kwa mfano unaweza kusema,…siku hizi hatufurahii tendo kama zamani, naona tunachoka, kumaliza haraka ila nahisi kama wewe mwenzangu ndiyo unachoka sana.

“Jifanye kama unamuuliza ili usikie anasemaje upate pa kuingilia…”Sijui tunaweza kuangalia kama kuna kitu kinachoweza kusaidia turudi kama zamani, nimekumbuka sana namna tulivyokuwa tunamaliza saa kadhaa tukivinjali miili yetu.” Hii inafungua mlango wa mazungumzo yasiyo na aibu na yeye hatohisi kudhalilishwa.

Mazungumzo yake yatakupa mwanga kuwa hata yeye amegundua kuna jambo halipo sawa. Sasa kwa kuanza kabla hamjakwenda hospitali mkutanishe na mshauri wa masuala ya kisaikolojia azungumze naye kwa kina na amueleze hali inayojitokeza sasa mkiwa faragha, kama hatojali nenda naye ili ukamsaidie kujieleza kwa uzoefu wako kwake. Mtaalamu wa saikolojia akizungumza naye atakushauri kwenda hospitali kutokana na atakachokibaini kama kinahitaji tiba nyingine zaidi.

Si rahisi lakini wakati haya yote yanaendelea usitake awe malaika kila akikosea kama binadamu unamtishia kuhusu tatizo lake. Kumbuka kuwa kila ndoa inahitaji uvumilivu na maelewano.

Ukikabiliana na tatizo kwa uwazi na huruma, mume wako ana uwezekano mkubwa wa kujitahidi kuboresha hali yake, na wewe pia kupata furaha kuwa naye faragha. 

Muhimu zaidi usithubutu kujadili suala hili mbele ya watu wengine hata kama ni ndugu zenu kwani mumeo atajihisi anadharauliwa na hakika utakuwa umemdharaulisha sana.

Pia hakikisha mnapokuwa wawili unazungumza naye mazungumzo kuhusu mahaba na namna anavyoijua kazi hiyo kiasi cha kukuteka na kukubali kuolewa naye huku ukimuhakikishia atakuwa sawa tena na mtaendelea kujilia vyenu.

Hii inamfanya mume wako ajisikie salama na kuondoa hofu au wasiwasi ambao pengine bila kujua alichangia kuathiri utendaji wake kitandani.

Nina uhakika dawa na tiba ya mumeo kuhusu suala lake wewe kwa kiasi kikubwa utasaidia kutokana na namna utakavyolichukulia suala hilo, na hakikisha anajua unasubiri kwa hamu awe sawa ili ujiachie utakavyo.

Kama alikuwa anatumia dawa za kuongeza nguvu bila shaka atamueleza mtaalamu wa saikolojia na mtatafuta tiba kuanzia hapo.