Pedro awashtukia waarabu, lazimakieleweke CAFCL

REKODI mbili zinaipa matumaini Yanga kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika leo wakati itakapoikaribisha JS Kabylie katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 1:00 usiku.

Rekodi hizo mbili ni za timu za Al Ahly na FAR Rabat zinazokutana leo huko Cairo, Misri ambazo matokeo yake yana nafasi kubwa kuamua kama Yanga itafuzu robo fainali au safari yake itaishia leo.

Kama ikiifunga JS Kabylie, Yanga itasonga mbele iwapo Al Ahly itapata ushindi wa nyumbani dhidi ya FAR Rabat kwa vile Yanga itafikisha pointi nane na hivyo itapenya kwa kubebwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Lakini kama FAR Rabat itapata ushindi au sare dhidi ya Al Ahly ugenini, Yanga itaishia katika hatua ya makundi hata kama itapata ushindi dhidi ya JS Kabylie leo.

Rekodi ya kwanza inayoipa matumaini Yanga leo ni ya Ahly kufanya vizuri katika mechi za Ligi ya Mabingwa ambazo inacheza ikiwa nyumbani ambapo katika michezo mitano iliyopita ya mashindano hayo, Al Ahly imepata ushindi mara nne huku ikitoka sare moja tu na imefunga mabao tisa huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Ukiondoa hiyo, rekodi nyingine ambayo inaweza kuipa Yanga imani kubwa ya kupenya leo ni ile ya FAR Rabat kutokuwa na makali ugenini pindi inapocheza katika mashindano hayo.

Hilo linaweza kuthibitishwa na mechi tano zilizopita za timu hiyo nje ya ardhi ya Morocco ambapo imeshinda mchezo mmoja tu, ikitoka sare miwili na kupoteza mechi mbili huku ikifunga mabao matatu tu huku yenyewe ikiruhusu mabao sita.

Hata hivyo katika mchezo wa leo, Yanga inapaswa ibadilike zaidi katika safu zake za ulinzi na ushambuliaji ambazo zimeonekana kutocheza vizuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Yanga umeonekana katika mechi tano ilizocheza kwenye hatua ya makundi ambapo timu hiyo imefumania nyavu mara mbili tu lakini safu yake ya ulinzi imeonyesha udhaifu kwa kuruhusu kufungwa mabao manne.

Ikiwa Yanga itafanikiwa kufuzu, nyota wake watavuna kitita cha Dola 450,000 (Sh1.2 bilioni) kutoka kwa uongozi wa timu hiyo kama ahadi ya kuwahamasisha wafanye vizuri leo.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alisema wanafahamu wapinzani wao hawana presha na mechi kwa sababu hawana nafasi ya kufuzu hivyo kazi ipo juu yao.

“Mechi ngumu na tulijua ugumu wa kundi mapema na tunajua Kablyie hawana nafasi ya kufuzu hivyo tunahitaji kufokasi na tunajua hawana presha na hilo lipo kwetu,” alisema Goncalves.

“Nafahamu na wachezaji wanaelewa na wanajua wanakutana na timu yenye nguvu na tunaamini tunayo nafasi kwa sababu kila mechi tulitengeneza nafasi nyingi na tulizipoteza hizo nafasi kwa mechi ya kesho hatuhitaji makosa kwa sababu ni mechi ya kihistoria.”

Beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alisema: “Hatma inakuwa kesho sisi kama wachezaji tutafuata maelekezo kutoka kwa makocha wetu, mimi binafsi nazipenda mechi za aina hiyo kwa sababu zinakutambulisha mchezaji wa aina gani. Tunatambua mchezo wa kesho na tupo tayari kupokea maelekezo ya makocha tuone tunafanyaje, tunahitaji nidhamu na kujitolea kwa pamoja ili kufanikisha jambo hilo.”

Kocha wa JS Kablyie, Josef Zinnbauer alisema wanafahamu uhitaji wa Yanga kwenye mchezo huo hivyo anategemea mechi ngumu.

“Hatuna presha tunajua Yanga watacheza kwa ajili ya mashabiki zao lakini kwetu tunauhitaji mchezo huo, nategemea mechi ngumu kwa sababu Yanga wanauhitaji mchezo huo kushinda mabao mengi hivyo tunatarajia watashambulia sisi tumejipanga tumekuja hapa kwanza kupata ushindi na kuonyesha kiwango bora, “ alisema.

“Wachezaji wengi hawana uzoefu wengine ndio mara yao ya kwanza, mpira muda mwingine unahitaji nafasi moja tu kuitumia, tulipata nafasi moja kubwa kwenye mechi dhidi ya AS Far hatukuweza kufanya jambo kwa hiyo muda mwingine unahitaji bahati.”

Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Arthur Bada alisema wanaifahamu Yanga ni timu nzuri lakini kwa upande wao wamekuja kuonyesha kiwango chao na kuchukua pointi tatu.

“Ni mechi ya kuonyesha uzoefu wetu na kuwa siriazi, Yanga ni timu nzuri nawafahamu vizuri tutafanya kila kitu ili tuweze kushinda na tupo hapa kufanya kazi na kupata matokeo mazuri.”

Wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC leo watakuwa ugenini huko Morocco kukabiliana na Wydad Casablanca katika mchezo utakaoanza saa 11:00 kwa muda wa Tanzania.

Ushindi wa kuanzia mabao mawili au zaidi katika mchezo huo utaifanya Azam itinge katika hatua ya robo fainali.

Na huko Afrika Kusini, wawakilishi wengine wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Singida Black Stars watakuwa uwanjani kukabiliana na Stellenbosch, mchezo ambao utaanza saa 1:00 usiku.