:::::::::::
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime leo Jumapili Februari 15, 2026 amesema Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi na kuwafuatilia watu ambao wamesikika kwenye Kipande cha Video kilichosambaa kwenye Mitandao ya Kijamii, wakimuhamasisha mtoto mdogo wa kiume kuvuta sigara kwani kitendo hicho ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu za kijamii.
Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari na Msemaji huyo wa Polisi imesema uchunguzi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa, akitoa wito kwa yeyote anayewafahamu watu hao au mtoto huyo kulisaidia Jeshi la Polisi ili kuwafikia na kuokoa afya ya mtoto huyo aliyehamasishwa kuvuta sigara.
“Tunatoa onyo pia kwa watu wenye tabia za kufanya vitendo vya kikatili na vya unyanyasaji kama hivyo na vinavyofanana na hivyo kwa watoto kwa lengo lolote lile.” Imesema taarifa ya Polisi.
Kulingana na Polisi Makao Makuu, Dodoma, wapo wanaofanya hivyo kwa watoto wadogo kwa msukumo wa kupata wafuasi kwenye mitandao ya kijamii (followers) kwaajili ya mitandao yao, likiwataka wanaofanya hivyo kuacha mara moja kwani hatua zitakazofuata ni kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwani matendo hayo ni uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.
