Samia ateta na Naibu Katibu Mkuu UN

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amekutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed, akiisifu Tanzania kwa uimarishaji mifumo ya utatuzi wa changamoto kwa mazungumzo na maridhiano.

Kikao hicho ni mwendelezo wa vikao ambavyo Samia na wasaidizi wake wamekuwa wakivifanya na viongozi mbalimbali wa jumuiya za kikanda na kimataifa, kuimarisha uhusiano na ushirikiano.

Ukiacha kikao cha mkuu huyo wa nchi na Amina, Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameshakutana na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres.

Taarifa ya kikao hicho, imetolewa leo, Jumapili Februari 15, 2026, na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu. Wawili hao wamekutana Addis Ababa nchini Ethiopia walikokwenda kushiriki mkutano wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Afrika (AU).

Katika kikao hicho, Amina ameisifu Tanzania kwa kuimarisha mifumo ya taasisi na utatuzi wa changamoto kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.

Pia, ameitaja Tanzania kuwa nchi yenye historia ya amani na uthabiti, akieleza kuwa ni Taifa linalopaswa kuigwa na mengine katika eneo la amani.

“Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani barani Afrika,” amesema.

Mazungumzo hayo pia, yamegusia mageuzi ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, ushiriki wa vijana katika maendeleo na umuhimu wa kuimarisha uratibu kati ya UN na AU.

Kwa upande wa Rais Samia, ameeleza dhamira ya Tanzania kuendelea kutekeleza mageuzi ya kiuchumi, kiutawala na kuimarisha ushirikiano wa nchi na UN katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Amesema mageuzi hayo ni katika sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi ikiwemo afya, elimu, maji safi, usafi wa mazingira, na kupunguza umasikini.

“Amepongeza na kuthamini mchango wa UN na taasisi zake katika jitihada za pamoja za maendeleo nchini, hususan katika nyanja za ushirikiano wa kidiplomasia na msaada wa maendeleo katika sekta mbalimbali,” imeeleza taarifa hiyo.

Samia ameonesha utayari wa Serikali kumpokea mjumbe maalumu wa UN aliyeomba kuja nchini kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa UN, António Guterres.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa nchi, alishafanya mazungumzo na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Angola, João Lourenço, aliyekubali kufanya ziara ya kiserikali Tanzania na kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba mwaka 2026.

Katika mazungumzo yao walioyafanya Februari 13, mwaka huu, wawili hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya kihistoria na ushirikiano wa kimkakati kwa manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi wa pande zote.

Februari 14, mwaka huu Rais Samia alikutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dk Abiy Ahmed, kabla ya ufunguzi rasmi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika, uliojadili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kukuza biashara na uwekezaji.

Taarifa hiyo, imeeleza viongozi hao pia walibadilishana uzoefu kuhusu mwelekeo wa uchumi wa nchi zao, Ethiopia inalenga kukuza uchumi kwa asilimia 10.2, huku Tanzania ikitarajia kufikia ukuaji wa asilimia 6.5, kama sehemu ya jitihada za kuimarisha ustawi wa wananchi wa nchi zote mbili.

Februari 15, 2026, Samia alifanya mazungumzo na Rais wa Comoro, Azali Assoumani na kujadili kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda, hususan katika sekta za biashara, utalii, usafirishaji wa baharini na masuala ya usalama.

Rais Assoumani alimshukuru Samia kwa ushirikiano wa pamoja na mchango wa Tanzania nchini kwake, hususan katika kuimarisha huduma za afya, biashara na masuala ya usalama, akishukuru mchango wa Tanzania katika huduma za kibingwa za matibabu kwa wananchi wa Comoro.

Kupitia mazungumzo hayo, Rais Assoumani pia alionesha nia ya kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania na Rais Samia aliridhia ombi hilo.