TRA United mambo si shwari

MABOSI wa TRA United huenda wakaachana na kocha mkuu wa timu hiyo, Mrundi Etienne Ndayiragije, baada ya pande hizo zote mbili kutokuwa na maelewano mazuri kwa siku za hivi karibuni, jambo linalochangia mwenendo mbaya wa matokeo ya Ligi Kuu.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti Ndayiragije aliyewahi kuzifundisha Azam FC, KMC FC na Timu ya Taifa ya Tanzania, hafurahishwi na baadhi ya viongozi wa kikosi hicho kumuingilia katika majukumu yake ya ufundishaji.

“Ni kweli suala hilo lipo, lakini sio kwa kiasi hicho cha kusababisha mwenendo wetu mbaya, hasa ukizingatia na aina pia ya wachezaji tuliowasajili, sisi bado tuna imani naye kubwa na tumeshampa kila alichokihitaji,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema suala la uongozi kudaiwa kuingilia benchi la ufundi sio sababu ya kufanya vibaya kwa kikosi hicho, isipokuwa changamoto wanayopambana nayo ni kuhakikisha wanalipa fedha wanazodaiwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.

“Kuna wachezaji ambao hawajalipwa fedha zao za usajili za mwanzoni mwa msimu huu, sasa baada ya kusikia wenzao ambao pia wamesajiliwa dirisha la Januari 2026 wamelipwa, wameanzisha kimgomo ambacho tunapambana nacho,” kilisema chanzo hicho.

Timu hiyo imecheza mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kupata ushindi, ambapo kati ya hizo imechapwa tatu na kutoka sare mmoja tu, huku mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni dhidi ya KMC ilipoichapa kwa mabao 3-0, Januari 23, 2026.

Ndayiragije amejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Kenya Police FC ya Kenya, Oktoba 29, 2025, baada ya kudumu kwa siku 333, tangu ateuliwe kikosini humo, huku akikipa kikosi hicho ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ msimu wa 2024-2025.

Kocha huyo aliipa Kenya Police ubingwa huo ukiwa ni wa kwanza kwa kikosi hicho katika historia tangu kilipopanda daraja mwaka 2021, hivyo, kuzima utawala wa Gor Mahia iliyochukua mara mbili mfululizo kuanzia msimu wa 2022-2023 na 2023-2024.