Unataka maisha ya furaha na kuridhika?

Dar es Salaam. Maisha ya furaha na utoshelevu si matokeo ya bahati, bali ni zao la uamuzi na juhudi za makusudi anazofanya mtu kila siku.

Katika ulimwengu wa sasa wenye kasi, presha za maisha, kazi na uhusiano vimekuwa chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo kwa watu wengi.

Hata hivyo, wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa kuna mbinu rahisi na zinazotekelezeka zinazoweza kumsaidia mtu kuishi maisha yenye utulivu wa nafsi na kuridhika.

Moja ya hatua muhimu kuelekea maisha yenye furaha ni uwezo wa kutambua na kudhibiti vyanzo vya msongo wa mawazo. Vyanzo hivi, vinavyofahamika kama visababishi vya msongo, hutofautiana kati ya mtu na mtu.

Kwa baadhi ya watu, msongo husababishwa na shinikizo la kazi, matatizo ya kifedha au changamoto za uhusiano, huku kwa wengine hali za kila siku kama foleni za barabarani au ratiba zisizo na mpangilio zikichangia hali hiyo.

Wataalamu wa saikolojia wanashauri kuwa ni muhimu mtu ajifunze kuisikiliza nafsi yake na kutambua mabadiliko ya kihisia yanayojitokeza kila anapokabiliwa na msongo.

Kuandika mawazo na hisia mara kwa mara ni mojawapo ya njia zinazosaidia kufahamu kinachosababisha msongo huo.

Baada ya kutambua chanzo, hatua inayofuata ni kupanga namna ya kukikabili. Hii inaweza kuhusisha kuweka vipaumbele, kupunguza majukumu yasiyo ya lazima na kupanga ratiba inayoruhusu mtu kuwa na muda wa kupumzika.

Kwa mfano, iwapo kuchelewa kazini kutokana na msongamano wa magari ni chanzo cha msongo, kuamka mapema na kuondoka nyumbani mapema kunaweza kusaidia kuepuka presha hiyo. Hatua kama hizi husaidia si tu kulinda afya ya akili, bali pia kuimarisha uhusiano na watu wengine kwa kuepuka hasira zisizo za lazima.

Mazoezi na mawasiliano silaha kuu

Mbali na kudhibiti vyanzo vya msongo, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara ni nguzo muhimu ya maisha yenye furaha.

Mazoezi husaidia kupunguza msongo wa mawazo kwa kuimarisha utendaji wa ubongo na kuifanya miili yetu kutoa homoni zinazochangia hisia za furaha na utulivu.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa mazoezi husaidia kupunguza mabadiliko ya ghafla ya hisia, kuongeza kujiamini na kupunguza dalili za sonona na hofu.

Aidha, mazoezi husaidia kudhibiti uzito wa mwili, kuboresha usingizi na kupunguza hatari ya magonjwa sugu kama ya moyo, shinikizo la damu na kisukari.

Shughuli rahisi kama kutembea kwa kasi, kukimbia, kuogelea, kuendesha baiskeli au kucheza muziki zinaweza kufanyika bila gharama kubwa.

Mazoezi yanayohusisha mwili na akili kwa pamoja, kama yoga na kunyoosha viungo, yameonekana kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza msongo wa mawazo.

Kuanza na kumaliza siku kwa kunyoosha mwili na kupumua kwa kina ni mbinu rahisi ambayo mtu yeyote anaweza kuifanya nyumbani bila msaada wa vifaa maalumu.

Hatua hizi ndogo, zikifanywa kwa uthabiti, husaidia kuifanya miili na akili kuwa katika hali ya utulivu.

Wataalamu wanashauri mtu asisite kushauriana na daktari iwapo atahisi mabadiliko yasiyo ya kawaida anapoanza mazoezi.

Pamoja na mazoezi, kushirikisha hisia ni jambo jingine muhimu katika kudumisha afya ya akili. Kuficha hisia na kuacha maumivu ya ndani yajikusanye,  huongeza mzigo wa kihisia na kuathiri ustawi wa mtu.

Kuongea na marafiki, ndugu au wafanyakazi wenzako husaidia kupata mtazamo mpana zaidi wa changamoto zinazokukabili. Kuomba msaada pale unapozidiwa si ishara ya udhaifu, bali ni hatua ya ujasiri na kujijali.

Wataalamu pia wanapendekeza kuandika hisia zako kila siku au kuzungumza na mshauri wa kisaikolojia inapobidi.

Njia hizi husaidia kupunguza mzigo wa mawazo na kujenga uwezo wa kudhibiti hisia.

Hatimaye, maisha ya furaha na utoshelevu huanza pale mtu anapochukua jukumu la kuitunza nafsi yake kimwili, kihisia na kisaikolojia.