…………
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wananchi wanazielewa sheria za nchi kwa kuzitafsiri katika lugha ya Kiswahili, hatua inayolenga kuongeza uelewa, uwajibikaji na upatikanaji wa haki kwa kila Mtanzania.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya sheria kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu, Utafiti na Mafunzo, Bi. Rehema Katuga, amesema kuwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, wizara zenye dhamana ya sheria husika na vyombo vya habari utasaidia kuhakikisha taarifa za kisheria zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati
“Tunaamini tukishirikiana na wadau wetu wote, ikiwemo wizara na vyombo vya habari, tutaongeza uelewa wa sheria kwa wananchi. Wakizijua haki zao wataweza kuzidai na kuzisimamia,” amesema Bi. Katuga.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa waandishi wa habari kufahamu msingi wa sheria kabla ya kuripoti masuala ya kisheria, ili kuepusha upotoshaji na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi.
Bi. Katuga ameeleza kuwa jukumu la uandishi wa sheria ni la kikatiba chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa mujibu wa Ibara ya 59(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayomtaka kuishauri Serikali katika masuala yote ya kisheria.
Majukumu hayo yanahusisha masuala ya Katiba na haki za binadamu, madai, jinai, mikataba pamoja na uandishi wa sheria.
Amefafanua kuwa tangu mwaka 2005, Serikali imekuwa ikifanya maboresho ya kimuundo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria. Mwaka 2018 zilianzishwa taasisi zinazojitegemea, ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, ili kuongeza ufanisi.
Hatua nyingine muhimu ilifanyika mwaka 2023 kwa kuanzishwa rasmi kwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, ambayo ndiyo ofisi pekee nchini yenye mamlaka ya mwisho ya kuandaa na kupitia rasimu za sheria kabla hazijawasilishwa katika hatua zinazofuata.
“Hata kama rasimu imeandaliwa sehemu nyingine, lazima ifike kwa Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa ajili ya mapitio na uthibitisho wa ubora,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa ofisi hiyo pia inaendesha mafunzo ya uandishi wa sheria kwa mawakili wa serikali, kwa njia ya mtandao na mikutano ya ana kwa ana, ili kuhakikisha rasimu zinazoandaliwa zinakidhi viwango vya kitaaluma kabla ya kuwasilishwa.
Kwa upande wa urekebu wa sheria (Law Revision), Bi. Katuga ameeleza kuwa ni mchakato wa kuunganisha marekebisho yote yaliyofanywa katika sheria mbalimbali ili kurahisisha usomaji na matumizi yake.
Amesema urekebu husaidia kuleta urahisi, kuongeza uzingatiaji wa sheria na kupunguza mianya ya rushwa.
Naye Mkurugenzi wa Divisheni ya Ufasili wa Sheria Bwana Said Ally Nzori, amesema tafsiri ya sheria inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anaielewa sheria kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya Katiba inayozungumzia usawa mbele ya sheria.
“Sheria huwa na katazo. Ili mtu apelekwe mahakamani, lazima awe amekiuka katazo lililoainishwa wazi katika sheria. Ndiyo maana ni muhimu wananchi waielewe sheria kwa lugha wanayoimudu,” amesema Bwana Nzori.
Ameeleza kuwa ofisi hiyo inatafsiri sheria kuu zinazopitishwa na Bunge pamoja na sheria ndogo zinazotungwa na taasisi na mashirika ya serikali takribani 288. Aidha, hutafsiri hukumu za mahakama, mikataba ya kimataifa na nyaraka rasmi zinazohitajika na mataifa mengine.
Mbali na hilo, ofisi huandaa miongozo na taratibu za uandishi na tafsiri ya sheria, pamoja na kuchapisha nyaraka za kisheria katika Gazeti la Serikali ili kuhakikisha ubora na upatikanaji wake kwa umma.
Hatua ya kutafsiri sheria zote kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili inatajwa kuwa chachu ya demokrasia na maendeleo endelevu, kwa kuwa sheria hutungwa kwa ajili ya kutumiwa na wananchi wote.
Kupitia maboresho hayo, Serikali inalenga kuhakikisha sheria si nyaraka za kitaalamu pekee, bali ni nyenzo inayoeleweka na inayowezesha kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa linalozingatia utawala wa sheria.




