Vitendea kazi vyatajwa kikwazo mfumo anuani za makazi

Unguja. Licha ya mafanikio kadhaa yaliyopatikana kwenye mfumo wa anuani za makazi, uhaba wa vitendea kazi umetajwa kuwa moja ya changamoto kubwa katika kuleta ufanisi zaidi katika kazi hiyo.

Hayo yamebainika wakati wa ugawaji wa vishikwambi kwa masheha, magari na bajaji za umeme kwa wafanyakazi wa Posta Kanda ya Zanzibar ikiwa ni mkakati wa kuongeza ufanisi katika mfumo wa anuani za makazi na utoaji huduma za kidijitali.

Mkurugenzi Msaidizi wa Anuani za Makazi, Edith Turuka akizungumza Februari 14, 2026 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania, Mohamed Khamis Abdulla amesema mfumo wa anuani za makazi ni nyenzo muhimu katika kuufikia uchumi wa kidijitali kwa kuunganisha mtoaji na mpokea huduma katika mnyororo mmoja wa utoaji huduma kwa haraka na ufanisi.

“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado zipo changamoto ikiwemo uhaba wa vitendea kazi kwa watendaji wa Serikali za mitaa. Hivyo, Serikali imenunua jumla ya vishkwambi 3,482 kwa ajili ya watendaji wa kata, mitaa, vijiji na shehia ili kuimarisha utekelezaji wa mfumo huo,” amesema Turuka.

Kati ya vishikwambi hivyo, Zanzibar imepewa vishikwambi 409 katika shehia 388 zilizopo Unguja na Pemba.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Fatma Mabrouk amesema zaidi ya anwani za makazi 500,000 tayari zimesajiliwa, jambo linaloonyesha mwitikio mzuri wa wananchi na manufaa ya mfumo huo katika matumizi ya kila siku.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya Tehama, kununua magari 12 na bajaji za umeme 40 kwa ajili ya kuboresha huduma za posta nchini.

“Hivi vifaa vitagawiwa katika shehia, halmashauri na mkoa ili kuhakikisha mfumo unatumika katika ngazi zote za utawala,” amesema.

Ili kuvitumia vishikwambi hivyo kwa ufanisi, Fatma amesema masheha watapatiwa mafunzo maalumu ya matumizi na utunzaji wake huku Serikali ikiendelea kuhakiki takwimu ili kuwa na mfumo sahihi, endelevu na unaochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Akikabidhi vifaa hivyo, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga amewataka watendaji wa Shirika la Posta Tanzania pamoja na masheha Zanzibar kutumia kikamilifu vitendea kazi hivyo ili kuharakisha utekelezaji wa mageuzi ya kidijitali na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Soraga, uanzishwaji na utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ni hatua ya kimkakati itakayorahisisha utambuzi wa makazi, maeneo ya biashara na taasisi, sambamba na kuimarisha huduma za posta, huduma za dharura na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

“Posta ni mdau muhimu katika utekelezaji wa mfumo huu kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika usambazaji wa barua, vifurushi na nyaraka rasmi. Ni lazima iendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya jamii ya sasa,” amesema Soraga

Amesema vifaa vilivyotolewa vitasaidia kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma, hususani katika maeneo ya vijijini na visiwani ambako upatikanaji wa huduma za posta umekuwa changamoto kwa muda mrefu.

“Kadhalika, vitachochea ukuaji wa biashara mtandaoni kwa kuwawezesha wananchi na wajasiriamali kutuma na kupokea bidhaa kwa uhakika zaidi, hatua itakayokuza uchumi wa kidijitali na kuongeza ajira kwa vijana,” amesema Soraga

Amesema “Hii ni hatua ya kuileta Serikali karibu na wananchi na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika safari ya kidijitali.”

Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Shirika la Posta Tanzania, Kanda ya Zanzibar, Halima Abdalla Hamad amesema taasisi hiyo imejipanga kuimarisha utoaji wa huduma na kuahidi kuvitumia vyema vitendea kazi vilivyokabidhiwa ili kuongeza ufanisi na kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aliwahimiza wananchi kuitumia posta ambayo kwa sasa imepanua wigo wa huduma zake na kutoa huduma mbalimbali kidijitali, akisisitiza kuwa posta ya leo ni zaidi ya kusafirisha barua, bali ni kiungo muhimu katika mnyororo wa biashara na huduma za kisasa.