Mwanza. Idadi ya wagonjwa wa saratani wanaotibiwa katika idara ya saratani ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando imeongezeka kutoka wagonjwa 320 mwaka 2009 hadi kufikia 2,000 kwa sasa, ikionesha ukubwa wa tatizo hilo mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Akizungumza leo Februari 15, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Saratani za Watoto Duniani yaliyofanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, Mkuu wa Kitengo cha Saratani na Daktari Bingwa wa saratani za watoto Bugando, Dk Hironima Joas amesema kati ya ongezeko hilo, watoto waliokuwa wakitibiwa mwaka 2009 walikuwa 50 pekee, lakini sasa wamefikia 400.
“Mwaka 2009 tulihudumia takribani wagonjwa 320 wakiwemo watoto 50. Idadi hii imekuwa ikiongezeka kila mwaka hadi kufikia wagonjwa 2,000 kwa sasa, wakiwemo watoto 400,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Saratani na Daktari Bingwa wa Saratani za Watoto Bugando, Dk Hironima Joas, akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Saratani za Watoto Duniani yaliyofanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Picha na Saada Amir
Amesema kufuatia ongezeko la wagonjwa wa saratani waliokuwa wakiripotiwa kutoka Kanda ya Ziwa mwaka 2017 walianza kutoa huduma za mionzi tiba, ambapo wagonjwa 101 walipatiwa huduma hiyo katika mwaka wa kwanza, hadi sasa wagonjwa 4,733 wamehudumiwa mionzi ya nje na 1,978 mionzi ya ndani.
“Kwa ujumla, tangu mwaka 2009 hadi sasa idara imehudumia wagonjwa 79,000 wakiwemo watoto 3,500 na sasa tunafuatilia wagonjwa 55,000 wakiwemo watoto 1500,” amesema Dk Joas.
Amesema kwa watoto, tatizo la saratani ni kubwa zaidi, akieleza kuwa takribani watoto 4,000 hukadiriwa kuwa na saratani na kati yao asilimia 50 hadi 60 hufariki dunia.
Amesema, kwa upande wa watu wazima, saratani zinazoongoza kwa wanaume Kanda ya Ziwa ni saratani ya tezi dume na koo, huku kwa wanawake zikiwa ni saratani ya shingo ya kizazi na matiti.
Ameeleza kwa upande wa watoto saratani zinazoongoza ni saratani ya tezi, damu, jicho na saratani ya tumbo ambayo mtoto anavimba figo akiwatoa hofu wazazi kuwa, saratani hizo zote zikiwahiwa mapema watoto wanaweza kupona.
Wakazi jijini Mwanza wakiendelea kupata huduma ya uchunguzi wa magonjwa wakati wa maadhimisho ya siku ya Saratani za Watoto Duniani yanayofanyika leo Februari 15, 2026 katika uwanja wa Nyamagana. Picha na Saada Amir
Dk Joas amesema kwa kushirikiana na wadau, Bugando imeboresha huduma kwa kuongeza majengo, vifaa tiba, mashine za mionzi, mashine maalumu za kugundua saratani za damu na vifaa vya kuchunguza vinyama.
“Sasa majibu ya vinyama yanapatikana ndani ya siku tatu hadi tano. Kwa saratani ya damu kwa watoto, ambayo awali tulikuwa tunasafirisha vipimo na kusubiri majibu kwa siku 21 hadi mwezi, sasa tunapata majibu ndani ya saa 24 hadi 72,” amesema.
Amesema kwa sasa idara ina watumishi 117, wakiwemo madaktari bingwa wa saratani tisa, daktari bingwa bobezi mmoja wa saratani za watoto, wauguzi bingwa watatu, na watumishi 23 waliopo masomoni.
Chanzo na kinga ya saratani
Daktari Bingwa wa saratani za watu wazima, Dk Cepheline Idrisa amesema saratani husababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo urithi wa familia, mtindo wa maisha kama uvutaji sigara, unywaji pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi, ngono isiyo salama, kushuka kwa kinga ya mwili, kemikali za viwandani na mionzi.
“Zipo sababu zisizozuilika kama historia ya familia. Kama baba alikuwa na saratani, ni muhimu mtoto kuchunguza mapema,” amesema.
Amesema dalili hutegemea sehemu ilipo saratani, lakini uvimbe usio wa kawaida kuanzia kichwani hadi miguuni unapaswa kuchunguzwa haraka hospitalini, akieleza matibabu hutegemea aina ya saratani na yanaweza kuwa upasuaji, dawa (kemo) au mionzi.
Amesisitiza umuhimu wa chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi, lishe bora ya matunda na mboga za majani na kuzingatia ngono salama.
Mashujaa wa saratani wasimulia
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Buzuruga, Stella Herman, amesema aliwahi kuugua saratani ya utumbo mpana na baadaye ya pafu, lakini hakukata tamaa.
“Saratani inatibika na kupona kabisa, hata ikirudi. Mwaka 2025 niligundulika tena na saratani ya pafu…nilifanyiwa upasuaji na baadaye kemo sasa nimepona kabisa,” amesema.
Naye Vanesa David, mmoja wa watoto waliopona saratani ya mishipa ya damu, amewataka wazazi kutowakatia tamaa watoto wao, akisisitiza kufuata maelekezo ya wataalamu na kuhudhuria kliniki.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Bugando, Dk Alicia Massenga, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Saidizi, Dk Cosmass Mbulwa amesema hospitali inaendelea na kampeni za elimu kwa jamii, uchunguzi wa mapema na utoaji wa chanjo, pamoja na ununuzi wa mashine na vifaa tiba.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Leba, akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Saratani za Watoto Duniani yaliyofanyika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Picha na Saada Amir
Hata hivyo, ametaja changamoto zilizopo kuwa ni uchache wa vifaa tiba, ukosefu wa mashine ya kisasa ya mionzi tiba, uhaba wa madaktari bingwa bobezi, kuongezeka kwa wagonjwa wasio na uwezo wa kulipia matibabu na upungufu wa fedha za kampeni za uchunguzi wa mapema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Leba amewataka wananchi kujiandikisha na kuwa na bima ya afya pamoja na kufanya uchunguzi mapema, akibainisha kuwa saratani nyingi za watoto hazina chanjo maalumu.
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa amesema Serikali imekamilisha wodi ya wagonjwa wa saratani Bugando na inaendelea kutoa msamaha kwa wagonjwa wasio na uwezo ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora.