Dar es Salaam. Wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wameangazia suala la amani na usalama katika bara la Afrika, huku wakibainisha hali siyo shwari kutokana na vitisho mbalimbali vilivyopo.
Hayo yamebainishwa leo Februari 16, 2026 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati akizungumzia ziara ya kikazi ya siku nne ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ethiopia kuanzia Februari 12 – 15, 2026.
Katika ziara hiyo, Rais Samia alihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Afrika, uliokuwa na dhima kubwa ya kuangazia hali ya amani na usalama barani Afrika pamoja na masuala mengine mtambuka.
Akizungumzia mjadala kuhusu usalama, Balozi Kombo amesema hali ya amani na usalama siyo shwari barani Afrika, kwani linapitia wimbi la mitihani, linalotokana na mambo mbalimbali ikiwamo ushindani wa rasilimali zilizopo barani Afrika.
Amesema ulimwenguni kote, Afrika ndilo bara pekee linaloonekana kuwa limebaki na rasilimali nyingi zaidi kuliko jingine lolote duniani, jambo linalochochea ushindani wa mataifa ili kuzifikia rasilimali hizo.
“Kwa maneno mengine, Afrika ni bara tajiri kuliko lolote duniani. Ukichukua utajiri wa wingi wa maji, rutuba kwenye ardhi, hali ya hewa hii ya oksijeni tunayovuta, Afrika inaongoza kwa sababu sisi ni wachafuzi wa mazingira kwa asilimia 2.4 tu,” amesema.
Ameongeza kuwa katika ajenda hiyo, ilizungumziwa migogoro inayoendelea kuongezeka na kukua na migogoro ya muda ya muda mrefu, zaidi ya miaka 10, 20 au 30 na inazidi kuendelea hadi hivi sasa.
“Miongoni mwa migogoro iliyochukua chati za juu ni Somalia kwa sababu juzi kumezuka mgogoro mwingine. Katika nchi hiyo, kuna watu wamejitenga na kusema ni eneo lao na baadhi ya nchi duniani zimeitambua nchi ndani ya nchi. Huo ni mgogoro mkubwa unaoendelea,” amesema.
Mgogoro wa pili unaobadilika mfumo wake, amesema ni Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwani watu ni haohao, kabila ni hilohilo, utamaduni ni huohuo, lakini mipaka kutofautiana kati ya nchi tatu na uwepo wa rasilimali nyingi katika eneo hilo.
Mbali na hiyo, Balozi Kombo ametaja mgogoro wa tatu kuwa ni ule wa mafahari wawili wa Sudan, kila mmoja akipigania kuliongoza taifa hilo ambapo kuna viashiria vya kugawanyika, lakini AU inafanya jitihada kulinusuru.
Balozi Kombo ameeleza kwamba wakuu wa nchi walijadili pia suala la ugaidi barani Afrika hususani katika jimbo la Cabo Delgado na Msumbiji, Pembe ya Afrika, jambo linalotatiza shughuli za kibiashara.
Waziri huyo aliongeza kwamba mwaka 2029, Tanzania inatarajia kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, nafasi ambayo itaipa fursa ya kulisemea bara hili kuhusu masuala ya amani na usalama.
“Tanzania imekuwa ni mjumbe wa Baraza la Usalama na Amani la AU kwa miaka minne mfululizo na mwaka 2029, Mungu akitujalia, Tanzania itakuwa ni mjumbe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” amesema Balozi Kombo.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema pembezoni mwa mkutano wa wakuu wa nchi, ulifanyika mkutano wa masuala ya fedha katika bara la Afrika kuangalia namna watakavyotafuta fedha kwa ajili ya sekta ya afya.
“Suala la muhimu lilikuwa ni kuangalia jinsi gani Wizara ya Fedha zitashiriki katika ugharamiaji wa huduma za afya. Tunafahamu umuhimu wa sekta ya afya, ni sekta inayochochea maendeleo na ustawi wa nchi zetu,” amesema.
Ameongeza kuwa kwenye mkutano mwingine ambao Rais wa Ghana ndiyo kinara wa fedha, walijadili namna upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Amesema bado kuna kazi kubwa ya kuimarisha miundombinu licha ya hatua kubwa ambayo Tanzania imepiga.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew amesema katika mkutano huo, wakuu wa nchi waliupitisha mwaka 2026 kuwa ni mwaka wa maji Afrika kwa sababu ni rasilimali inayokwenda kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uzalishaji hasa kilimo.
Amesema ajenda2063 ni dira ya Afrika inayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi hususani kupitia sekta ya kilimo cha umwagiliaji. Amesisitiza kuwa ili kuimarisha usimamizi endelevu na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, upatikanaji wa maji ni muhimu.
“Sekta ya maji ni kichocheo cha maendeleo endelevu kwani maji ndiyo yanatumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Serikali imeweka misingi thabiti ya ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maji,” amesema Kundo.