Beki Bigman matumaini kibao Championship

BEKI wa kati wa Bigman FC, Better Abdallah Mnyamisi, amesema licha ya kukitumikia kikosi hicho kwa muda wa mwezi mmoja tangu ajiunge nacho akitokea, IAA ya jijini Arusha inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, ila anafurahia maisha yake mapya.

Nyota huyo alijiunga na IAA baada ya kuachana na TMA ya jijini Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship, ambapo alifikia makubaliano ya kusaini mkataba wa miezi sita na Bigman hadi mwisho wa msimu, ili kuitumikia timu hiyo ya Mkoa wa Lindi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mnyamisi, amesema licha ya ugeni wake katika timu hiyo ila anafurahia mapokezi mazuri ambayo ameyapata kutoka kwa wachezaji wenzake, akiahidi kupambana zaidi ili azidi kushawishi benchi la ufundi la kikosi hicho.

“Jambo ninalofurahia ni uzoefu wangu katika Ligi ya Championship, nimeanza maisha mapya lakini nimeaminiwa moja kwa moja na benchi la ufundi, hali inayonipa morali zaidi ya kupambana kwa ajili ya timu na malengo yangu pia,” amesema Mnyamisi.

Nyota huyo licha ya kuichezea Championship msimu wa 2024-2025, ila ana uzoefu mkubwa pia wa kucheza Ligi Kuu Bara, kwani aliwahi kuitumikia Polisi Tanzania kuanzia msimu wa 2021-2022 hadi 2023-2024, kisha kuondoka na kujiunga rasmi na TMA.

Msimu wa 2024-2025, nyota huyo aliiwezesha TMA kumaliza Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya tano na pointi 53, baada ya kushinda mechi 15, sare minane na kupoteza saba kati ya 30, iliyocheza, huku ikifunga jumla ya mabao 40 na kuruhusu 29.