KIKOSI cha Yanga usiku wa jana kilikuwa uwanjani kupigania hatma ya kupenya kwenda robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, lakini mapema kocha mkuu wa timu hiyo, Pedro Goncalves amekiri kuna vitu ameviona kwa kiungo mpya Buba Jammeh.
Buba amesajiliwa dakika za lala salama za dirisha dogo lililofungwa mwezi uliopita na tayari kiungo huyo kutoka Gambia akiwa ameshaanza kujifua na wenzake mazoezini na ilitarajiwa huenda jana angekuwa sehemu ya kikosi cha Yanga dhidi ya JS Kabylie kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kukamilisha ratiba ya makundi kwa Kundi B.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro amesema mchezaji huyo amemfahamu miaka minne iliyopita hivyo anajua ubora wake ulivyo, japo alimpa ushauri wa baadhi ya mambo anayotakiwa kuyaongeza ili akae sawa na kuwasha moto kisawasawa.
Amesema, Buba ni mchezaji mgeni hapa Tanzania, anatakiwa kuonyesha ubora kwenye kila mchezo atakaopewa nafasi ya kucheza kuanzia mazoezini mpaka uwanjani.
“Ukiniuliza kuhusu Buba nitakwambia ni mchezaji mzuri sana, lakini sasa yuko ugenini, timu mpya kabisa ambayo hajawahi kuichezea, hivyo kuna kitu anatakiwa kukionyesha cha ziada,” amesema Pedro na kuongeza;
“Jambo la kwanza ambalo hata yeye nilimweleza ni kwamba anatakiwa kujituma. Namfahamu vyema kwa miaka kama minne, lakini nimemwambia amejiunga na timu kubwa hapa Tanzania, anatakiwa kuonyesha uwezo wake bora kwenye kila mchezo atakaokuwa uwanjani.
“Buba ana uwezo wa kufanya makubwa hapa Yanga kama akiwa na juhudi zaidi, kwa sababu atakutana na ushindani wa namba, ambapo hiyo ndiyo itakuwa kazi yake ya kwanza ya kufanya.”
Buba mwenye umri wa miaka 24 ametua Yanga akitokea Interclube ya Angola ambayo ameichezea kwa msimu mmoja pekee na kote akiingia dirisha dogo na kutoka muda huo huo msimu uliofuata, huku akiacha rekodi ya kufunga mabao manne pekee.
Kutoka Ligi ya Angola, Interclube msimu huu haina rekodi nzuri kwani inashika nafasi ya 11, ikicheza mechi 14 ikifikisha jumla ya pointi 16, huku kinara akiwa nazo 36 katika mechi 14.
Mgambia huyo anakwenda kuchukua nafasi ya Moussa Balla Conte aliyetolewa kwa mkopo na kwenda Raja Casablanca ya Morocco, timu anayoifundisha kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids.
Conte aliondoka kutokana na ugumu wa namba pale Jangwani na sasa kuna maswali wanajiuliza mashabiki wa Yanga, kwamba Buba atatoboa mbele ya mastaa kadhaa waliopo kama Pacome Zouzoua na wengine ambao tayari ameshapenya kwenye hesabu za kocha huyo Mreno.