CHANDE ASISITIZA MASHIRIKIANO NA UBUNIFU KUKUZA SEKTA YA MALIKALE

Na Saidi Lufune, Dodoma
NAIBU  Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amehimiza Idara ya Maliakale kuongeza ubunifu katika kutangaza vivutio vya maliakale na makumbusho ya kihistoria ili kuvutia watalii wengi wa ndani na nje ya nchini.
Mhe. Chande amebainisha hayo jijini Dodoma katika kikao kazi na Idara ya Malikale ambapo amefafanua kuwa sekta ya maliakale nchini inapaswa kuwa juu na kuwa sehemu ya kuchangia ukuaji wa mapato katika ukuaji wa uchumi wa Taifa hususan katika kufufua maeneo mapya ya utalii wa malikale na makumbusho ya kihistoria
Aidha, ameiagiza idara hiyo kuongeza mashirikiano yenye tija na Wizara ya Utalii na Mambo ya Malikale ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kuongeza nguvu katika kutangaza mazao mapya ya vivutio vya Maliakale huku akisisitiza uhifadhi wa makumbusho ya nyimbo zitokananazo na matukio ya historia ya Taifa wakati na baada ya ukombozi wa Tangangika na Zanzibar.
Awali akiwasilisha taarifa za idara hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Malikale Dkt. Christowaja Ntandu amebainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Maliakale itaendelea kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kufungua maeneo na vivutio vipya vya Malikale; kuendelea kutangaza na kuhamasisha jamii kupitia maonesho, matamasha na warsha juu ya umuhimu wa kuwekeza na kutumia rasilimali za utamaduni kama zao mojawapo la utalii hapa nchini.