Dk Mwigulu aonya wageni kuanzisha kampuni kwa kivuli cha wazawa

Tanga. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amekagua mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani mkoani Tanga huku akionya wageni wanaokuja nchini na kuanzisha kampuni kwa kutumia kivuli cha wazawa.

Pia, ameeleza kufurahishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo ambao, unatajwa utakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa mataifa hayo mawili na kupunguza bei ya mafuta.

Dk Mwiguli ameyasema hayo leo Jumatatu, Februari 16, 2026 wakati akikagua mradi huo utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 5.65 ni kielelezo cha undugu kati ya Tanzania na Uganda. “Ninatambua msisitizo uliowekwa na viongozi wetu, Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Yoweri Museveni katika utekelezaji wa mradi huu.”

Dk Mwigulu, ambaye yuko mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi amesema Serikali itaendelea kuweka uzito unaostahili katika kutekeleza mradi huo ambao umefikia asilimia 81 ya utekelezaji kwa heshima ya undugu kati ya Tanzania na Uganda.

“Lakini tutaendelea kuweka uzito unaostahili kwa heshima ya kulinda uhuru wetu kwa kuwa ni nchi huru ambayo inaweza kujitegemea kutekeleza mradi wa kiwango hiki, hiki ni kielelezo kwamba nchi yetu inaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na miradi mikubwa ya maendeleo.”

Kuhusu wageni kuanzisha kampuni kwa kivuli cha wazawa, Dk Mwigulu ameonya watu wanaoanzisha kampuni na kuziita za wazawa huku nyuma yakimilikiwa na wageni ili kunufaika na fursa ya ‘Local Content’ ya ushirikishwaji wa Watanzania kwamba watakaogundulika watafungiwa na hawatafanya kazi tena nchini.

“Wapo wasio waaminifu wanawatumia Watanzania kuanzisha kampuni wanasema ni ya wazawa. Tunataka kuinua kampuni za Watanzania, upo mchezo mgeni anatumia anuani ya Mtanzania ambaye si mnufaika, wale watakaogundulika wanafanya ujanja tutawafungia na hawatafanya kazi tena kwetu,” amesema.

Dk Mwigulu amesisitiza kuwa kufanya hivyo ni kuwatapeli Watanzania na kuwaibia fursa. “Tumekupa mradi una nafasi yako tena asilimia kubwa, tunataka hiyo sehemu ndogo inawanufaishe Watanzania na ninyi mnawaibia, wale tuliowapa kazi ya kufuatilia hili tukigundua upo huu mchezo tutakuchukulia hatua kwa kuwa tutajua na wewe ni sehemu yao.”

Kadhalika, Dk Mwigulu ameagiza wasimamizi wa mradi huo wahakikishe kuwa baada ya ujenzi huo kukamilika kipaumbele cha ajira kitolewe kwa wale waliofanya kazi kwenye mradi huo kwa kuwa wanakidhi vigezo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema kuwa mradi huo ambao ulianza utekelezaji wake mwaka 2022 na unategemea kukamilika ifikapo Julai 2026 na Serikali ya Tanzania ni mwanahisa kwa asilimia 15.