Gamondi asani miwili Taifa Stars, akiahidi raha

KOCHA Miguel Gmondi amehakikishiwa maisha Taifa Stars baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuinoa, huku akiwaahidi mashabiki wa soka nchini furaha kuliko ile ya kucheza 16 Bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.

Gamondi aliyekuwa kaimu kocha mkuu wa Stars akichukua nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliiwezesha kutinga hatua ya 16 Bora Afcon iliyomalizika mwaka huu huko Morocco ikitolewa hatua hiyo kitatanishi na wenyeji waliopoteza mechi ya fainali mbele ya Senegal.

Mkataba wa miaka miwili aliopewa Gamond ni wa mahsusi kuhakikisha bendera ya taifa inapeperushwa vyema michuano mbalimbali ikiwemo ya fainali za Afcon 2027 zitakaofanyika kwa ushirikiano Tanzania, Kenya na Uganda.

Baada ya kusaini, Gamondi amesema: “Ni jukumu langu kuhakikisha timu inafanya vizuri na kuleta sifa kwa Tanzania na mashabiki kufurahia. Nipo tayari kufanya kazi hiyo. Nashukuru mashabiki kuniunga mkono.”

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema  serikali imewekeza pesa katika soka ili kumwezesha kocha kuandaa programu ya muda mrefu kuwafundisha wachezaji.

“Kwa sasa timu ni mali ya Gamondi. Kasaini mkataba wa miaka miwili,” amesema Makonda.

“Baraza la Michezo Tanzania (BMT), lifanye tathimini ya kina ya kwa nini mashirikisho mengine ya michezo hayaleti mataji nchini, tunahitaji yote yafanye kazi isiwe soka pekee, awamu nyingine nikija katika mkutano mazungumzo iwe ya shirikisho lingine.

“Ifikie hatua ngumi siku aje aletwe Mike Tyson kuamua ngumi, lengo ni kuona vijana wengi wanapata ajira katika michezo mbalimbali ili kuendesha maisha yao na hilo litaondosha ukosefu wa ajira kwa vijana.”

Pia alitoa maelekezo kwa Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Ngilangwa kuhakikisha anamaliza mchakato wa Simba kuhuasu suala la umiliki kwa kutumia kanuni na sheria, na kusiwepo sababu za kukwamisha.

“Nisingependa kuanza kutoa maoni na kuingilia mchakato. Simu kwetu zinapigwa sana na kama kuna kipindi cha kuzingatia kanuni na sheria ni hiki cha uongozi wangu. Hivyo mwezi huu uwape utaratibu Simba waendelee na mambo yao, simamia sheria na kanuni zinavyosema kusiwepo na mkwamo wa kiuongozi,” amesema.

Makonda alizipongeza Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars kufika makundi ya michuano ya CAF na kutolewa zikishindwa kwenda robo fainali akizitaka kujipanga zaidi msimu ujao ili zifike fainali.

Simba na Yanga zilikuwa zikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika zikiwa makundi ya B na D mtawalia, huku Azam na Singida zikicheza kwa mara ya kwanza hatua hiyo katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.