Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kiongozi lazima awe na juhudi binafsi na endelevu kujifunza ili kuendana na mabadiliko yanayojitokeza ikiwamo mbinu za kukabiliana na changamoto mpya.
Abdulla ameyasema hayo leo Februari 16, 2026 katika ufunguzi wa mafunzo ya kamati ya uongozi ya wabunge, tume ya utumishi wa wabunge na makamu wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge yaliyofanyika katika Ofisi ndogo ya Bunge Tunguu Zanzibar.
Hemed amesema mafunzo kwa viongozi huwasaidia kufanikisha uendeshaji wa Bunge sambamba na kuimarisha ushirikiano baina ya wabunge na Serikali katika kusonga mbele kiuchumi, kisiasa na kijamii.
“Uongozi ni dhamana, na kiongozi lazima uwe tayari kujifunza kila siku mbinu mpya ili kuendana na mabadiliko ya kidunia,” amesema Hemed.
Amesema Ibara ya 63 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imelipa uwezo Bunge kusimamia na kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa bajeti ya muda mrefu na mfupi, kutunga sheria zitakazosaidia utekelezaji wa masuala mbalimbali na kuridhia mikataba pamoja na kuuliza maswali yanayowagusa wananchi.
Kwa upande wa Tume ya Utumishi wa Bunge imepewa dhamana ya kusimamia utumishi wa bunge ikiwemo kusimamia bajeti, rasilimali za Bunge na kuangalia masilahi ya watumishi wa Bunge na wabunge.
Hemed amesema anaamini kuwa mafunzo hayo yatakuwa jukwaa muhimu ambalo litawapa fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza kwa pamoja na kujenga mtazamo wa pamoja kuhusu namna bora ya kuziendesha kamati zao kwa weledi, ufanisi na kuwawezesha kuwa na Bunge la viwango.
Amewasisitiza viongozi hao juu ya umuhimu wa kushirikiana kwa karibu kati ya Bunge, Tume ya Utumishi wa Bunge na Serikali katika kuhakikisha kuwa majukumu ya Bunge yanatekelezwa kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni ambazo huiwezesha Serikali kufanya majukumu yake kwa ufanisi.
Naye Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema katika mafunzo hayo wabunge watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wa kazi za Bunge na mustakabali mzima wa uongozi kwa lengo la kuwatumikia viongozi na wananchi kwa ujumla.
Spika amesema mafunzo hayo ya siku tatu, ambayo yameanzia mkoani Dodoma yatajadili mada mbalimbali ikiwemo madaraka, majukumu, mipaka na utendaji kazi wa kamati na uongozi wa kimkakati katika uendeshaji wa shughuli za Bunge.
Mada nyingine zitakazofundishwa na kujadiliwa katika mafunzo hayo ni uratibu na utekelezaji wa shughuli za Serikali katika kamati za Bunge, uhusiano na changamoto, haiba ya viongozi na itifaki ya kidiplomasia katika utekelezaji wa shughuli za kibunge na kiserikali ngazi ya kitaifa na kimataifa.