::::::
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika kusimamia mifumo ya kidijitali ya ufuatiliaji wa mabasi, ikisema hatua hizo zimeanza kuleta matokeo chanya katika kudhibiti ajali barabarani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya ziara ya kikazi katika ofisi za mamlaka hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jonhson Lutasingwa, alisema wamejionea maboresho makubwa ya mifumo ya udhibiti mwendokasi (VTS).
Hata hivyo, kamati hiyo imeitaka LATRA kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva wa mabasi, hususan ya masafa marefu, wanaobainika kuchezea au kuharibu mifumo hiyo kwa lengo la kukwepa udhibiti.
Lutasingwa alisema vitendo hivyo vinahatarisha maisha ya abiria na vinadhoofisha jitihada za Serikali za kupunguza ajali kupitia matumizi ya teknolojia.
Amesisitiza kuwa mamlaka hiyo inapaswa kuendelea kuimarisha ufuatiliaji na kuhakikisha wote wanaokiuka taratibu wanachukuliwa hatua bila upendeleo.
Aidha, kamati imeelekeza kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya LATRA na vyombo vingine vya usalama barabarani ili kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, amesema wamepokea maoni na maelekezo ya kamati hiyo na wataendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kuimarisha usalama katika sekta ya usafiri.









