Tanga. Watu watano wamepoteza maisha baada ya kufukiwa na kifusi katika machimbo ya mchanga ya Bolbit, Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.
Ajali hiyo ilitokea saa 11:30 jioni Februari 15, 2026, wakati watu hao wakiwa katika shughuli za uchimbaji wa mchanga.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema chanzo cha ajali hiyo ni kukatika kwa kingo za udongo zilizoporomoka na kuwaangukia wachimbaji hao.
Mchunguzi amesema, “Ngema ya udongo ilikatika ghafla na kuwafukia watu watano waliokuwa wakichimba, hali iliyosababisha vifo papo hapo.”
Jitihada za uokoaji zilihusisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi wa eneo hilo, ambapo miili ya marehemu ilifanikiwa kutolewa chini ya kifusi.
Miili hiyo imehifadhiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Korogwe Vijijini Makuyuni kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria na mazishi.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wanaojihusisha na uchimbaji kuzingatia kanuni za usalama kazini, likisisitiza kuwa, “Uzembe wa tahadhari unaweza kuzitumbukiza familia katika majonzi.”
Kadhalika, jeshi hilo limewataka viongozi wa vijiji na mitaa kusimamia kwa karibu shughuli za machimbo ili kuzuia majanga kama hayo.