Kihongosi atoa maagizo ujenzi chuo cha Veta Nzega

Tabora. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuharakisha utoaji wa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) wilayani Nzega mkoani Tabora.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu, Februari 16, 2026 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho kilichopo Kata ya Obada, Nzega.

Kihongosi amesema hadi sasa Serikali imetoa zaidi ya Sh500 milioni kwa ajili ya mradi huo, Sh484 milioni tayari zimetumika kujenga majengo ya utawala na karakana, akieleza kuwa ubora wa majengo hayo unaendana na thamani ya fedha zilizotolewa.

Amesema kinachosubiriwa kwa sasa ni fedha za ukamilishaji wa mradi, huku akibainisha kuwa changamoto ipo kwa upande wa wizara husika inayopaswa kupeleka fedha hizo. Ametumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Elimu kuharakisha utoaji wa fedha ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Katibu wa Nec, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi akizungumza na Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe.



Kihongosi amesisitiza kuwa lengo ni kuona wananchi wa Nzega wakianza kunufaika na uwekezaji huo, akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akielekeza miradi ya maendeleo ikamilike kwa wakati ili wananchi wapate huduma stahiki.

Amefafanua kuwa uwepo wa Veta Nzega utakuwa mkombozi kwa vijana wengi watakaopata mafunzo ya ufundi yatakayowawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu. Amesema chuo hicho kitatoa fani mbalimbali ikiwamo uashi, uselemala, udereva na uchomeaji, bila kujali kiwango cha elimu alichonacho mwanafunzi.

Aidha, amesema atawasiliana na wizara hiyo ili kuhakikisha fedha zilizobaki zinawasilishwa Nzega kwa wakati, akisisitiza kuwa Serikali tayari imeshatimiza wajibu wake wa msingi katika kuanzisha mradi huo.

Katibu wa Nec, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi akizungumza na wananchi wilayani Nzega mkoa wa Tabora.



Awali, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Nzega ambaye pia ni msimamizi wa mradi huo, Nicodemas Shirima amesema ujenzi umefikia asilimia 75, huku majengo tisa yakiwa tayari yamejengwa kwa fedha zilizopokelewa.

Amesema changamoto kubwa ni kuchelewa kwa fedha, hali inayosababisha kusimama kwa kazi mara kwa mara.

Hata hivyo, ameeleza kuwa wakipokea fedha zilizobaki, watakamilisha mradi huo kwa wakati ili uanze kutoa huduma kwa wananchi.

Baada ya kukagua mradi huo, Kihongosi aliendelea na ziara yake mkoani Tabora kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Stand ya Zamani, Nzega Mjini, alisikiliza na kushughulikia kero za wananchi ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake katika mkoa huo.