Lissu, ‘mfuasi’ wake walivyokabiliana mahakamani kesi ya uhaini

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekabiliana na anayedai kuwa mfuasi wake ambaye ni shahidi wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili, huku Lissu akieleza kuwa na mashaka naye kama kweli ni mfuasi wake.

Lissu na shahidi huyo wa Jamhuri aliyejitambulisha kama mfuasi wa Chadema na wa Lissu binafsi (Team Lissu), wakati wa mahojiano, ambapo Lissu amemuhoji maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake alioutoa mahakamani hapo.

Shahidi huyo ambaye ni miongoni mwa mashahidi fiche wa Jamhuri (waliopewa ulinzi, yaani wasiotakiwa kuonekana wala kutambulika), ametoa ushahidi akiwa ndani ya kizimba maalumu ambamo hawawezi kuonekana kwa wasikilizaji wala mshtakiwa, isipokuwa kwa majaji tu ametambulishwa kwa jina la P2 (34).

Lissu  anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa,

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu  linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Kwa mujibu wa shahidi  wake leo Jumatatu, Februari 16, 2026 akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Ignas Mwinuka , shahidi huyo wa saba, ni mkazi wa Matalawe, Songea, mkoani Ruvuma. Pia ni fundi umeme na ni mfuasi wa Chadema tangu mwaka 2021 na amekuwa akishiriki katika mikutano mbalimbali.

Aprili 4 , 2025 saa 4 akiwa katika mtandao wa kijamii wa Youtube, alikutana na video ya Lissu ya mkutano na waandishi wa habari, akieleza kuwa mwaka huu hakutakuwa na uchaguzi na kwamba waliokuwa wanataka kugombea udiwani, ubunge na urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wasahau.

Katika maelezo hayo Lissu alisisitiza kuzuia uchaguzi mkuu usifanyike kama namna ya kuleta mabadiliko na akawataka kila mmoja kuwa jasiri, na ujumbe huo ulimuhamasisha akajiandaa kukinukisha kuzuia uchaguzi huo kama Lissu alivyosema.

Katika maelezo  aliyoyatoa polisi, ambayo yamepokewa mahakamani kama kielelezo cha upande wa mashtaka, pamoja na mambo mengine alieleza kuwa  yeye ni timu Lissu, hata wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani ya chama uliomuweka Lissu katika uenyekiti, yeye alikuwa upande wake.

Pia alieleza kuwa baada ya kupata ujumbe wa Lissu wa kuzuia uchaguzi kwa kukinukisha alijiandaa kukinukisha.

Baada ya shahidi huyo kumaliza ushahidi wake alihojiwa maswali ya dodoso na Lissu.

Sehemu ya maswali na majibu ya dodoso

Lissu: Shahidi kwanza habari ya Matalawe, kwema?

Shahidi: Matalawe ni salama

Lissu: Waeleze majaji kama uliandika maelezo Polisi

Shahidi: Nilichukuliwa maelezo polisi.

Lissu: Ndio haya maelezo ya Aprili 22, 2025?

Lissu: Uliyasaini hayo maelezo yako na ukionyeshwa maelezo hayo utayatambua baba?

Shahidi: Ndio nilisaini na nikionyeshwa nitayatambua.

Lissu: Naomba Waheshimiwa majaji shahidi aonyeshwe maelezo yake.

Shahidi: Baada ya kupewa nakala ya maelezo, ndio yenyewe.

Lissu: Kwenye ushahidi wako uliulizwa unamfahamuje huyu Tundu Lissu na ukasema una mfahamu kutokana na mchango wake wa kisiasa sasa hayo maneno yapo katika maelezo yako ya onyo?

Shahidi: Sijasema ila mimi ni mfuasi wako.

Lissu: Shahidi umeieleza Mahakama kuwa kwenye hiyo video uliona mtandao wa Jambo Tv, inaelekeza Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema kuwa viongozi wanaotaka kugombea  udiwani, ubunge na urasi wasahau, hayo maneno yapo katika maelezo yako?

Lissu- Yako wapi? Maana wafuasi wangu huwa wana akili, sasa wewe unanitia wasiwasi.

Lissu: Sasa shahidi umesema wewe ni mfuasi wa Chadema, ni kweli au si kweli?

Lissu: Waeleza majaji kama wafuasi wa Chadema huwa wana alama usoni.

Lissu: Una kadi ya Chadema?

Lissu: Sasa waheshimiwa majaji watajuaje kama wewe ni mfuasi wa Chadema?

Shahidi: Sijui kwa ufahamu wao.

Lissu: Una utambulisho wowote wa uanachama wa Chadema?

Lissu: Sasa majaji wataaminije kama wewe ni mfuasi wa Chadema na si chawa wa Mama?… vicheko

Lissu: Umesema huwa unachangia shughuli za chama, ni kweli au si kweli

Lissu: Unajua kuwa michango ya Chadema huwa inatolewa kwa njia ya mtandao, tigopesa M-pesa na kadhalika, wewe una risiti au ushahidi wowote wa kuchangia michango hiyo?

Lissu: Sasa wewe huna risiti huna chochote cha kuthibitisha hiyo michango sasa mahakama itaaminije?

Lissu: Umeieleza mahakama kuwa uliona video la Lissu mitandaoni Aprili 4, 2025, umewaonyesha majaji hiyo video?

Lissu: Umeiwasilisha mahakamani hiyo video kama kielelezo?

Lissu: Sasa majaji watajuaje kama uliona hiyo video kama hujaiwasilisha mahakamani?

Shahidi: Wanaweza kuingia kwenye mtandao wa Jambo TV.

Lissu: Sasa majaji ndio wahangaike kwenda kuitafuta huko, umewapa bando? ( anahoji Lissu huku akicheka).

Lissu: Umesema ulikwenda Mfaranyaki kuuliza habari za kukamatwa kwa mwenyekiti wako na ukakamatwa, kwani kuuliza habari za kukamatwa kwa mwenyekiti wako na kujua habari za mkutano ni kosa la jinai?

Shahidi: Sifahamu sheria.

Lissu; Nimesema wafuasi wangu huwa wana akili lakini angalau kwa ufahamu wako hilo ni kosa?

Lissu: Umesema ulikamatwa kwa tuhuma za kuchochea kwani ulipokwenda Mfaranyaki (ofisi za Chadema) ulikwenda kuchochea?

Lissu: Ulikwenda kufanya vurugu?

Lissu: Ndio maana nasema wewe si mfuasi wangu, maana wafuasi wangu wana akili.

Lissu: Umesema ulikamatwa na kuhojiwa kwa tuhuma za uchochezi na kupanga kufanya vurugu, hayo mahojiano yako wapi?

Lissu: Ulipelekwa mahakamani?

Lissu: Hiyo kesi iliishia wapi?

Lissu: Kwa hiyo umekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuchochea na kupanga kufanya vurugu halafu baadaye yakaisha tu na ukawa shahidi, nini kilitokea?

Lissu: Shahidi kuna kiongozi yeyote wa Chadema aliyetishia kukua?

Lissu: Kuna mwanachama yeyote wa Chadema aliyetishia kukua?

Lissu: Umewahi kuandika maelezo yoyote polisi baada ya yale ya Aprili 22, 2025?

Lissu: Waeleze majaji kama tangu uandike maelezo ya onyo ya Aprili 22,2025 kama ulishawahi kufanya mawasiliano yoyote na Polisi.

Shahidi: Hapana, ila nimepigiwa simu Februari 11, 2026 wakinitaka kuja kutoa ushahidi Mahakamani.

Lissu: Kuna kiongozi au mwanachama yeyote wa Chadema aliyekutishia wewe kukua? Kukutishia kukuua kwa ajili ya kesi hii?

Shahidi: Kuna vitisho mitandaoni.

Lissu: Kuna kiongozi yeyote au mwanachama yeyote wa Chadema au mfuasi wangu aliyekutishia kwa namna yoyote ile kwa ajili ya kesi hii?

Lissu: Siku ya Aprili 7, 2025 uliwahi kuwa na mwandishi wa Jambo TV?

Lissu: Siku hiyo wewe na mwandishi wa Jambo TV mliwahi kwenda makao makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma mkakutana na askari polisi anaitwa Andrew Churi?

Lissu: Nakuuliza hivyo kwa sababu kuna maelezo hapa yanasema wewe na P, mlikwenda Polisi makao makuu Dodoma mkakutana na askari Andrew Churi.

Lissu: Sasa ieleze mahakama kama kweli mlikwenda kukutana na huyo askari Andrew Churi.

Lissu: Naomba uwaeleze majaji kama ulishuhudia makabidhiano ya flash na memory kadi dhidi ya mwandishi  wa Jambo TV kwenda kwa Inspekta Churi.

Lissu: Waeleze majaji kama hotuba yangu ya Aprili 3, 2025 iliyokuhamasisha kama nilisema watu wakafanye fujo.

Lissu: Waeleze majaji kama kuhamasisha kuzuia uchaguzi kama ni kosa la jinai?

Lissu: Waeleze majaji kama ni kosa (yeye shahidi)  kuamini maneno ya mwanasheria nguli (yeye Lissu kama shahidi alivyomwelezea anavyomtambua).