MAHOJIANO MAALUMU: Wasira ataja muundo wa maridhiano, agusia kesi za kisiasa

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema kwa hali ilivyo muundo wa maridhiano unapaswa kuihusisha Serikali ili iiongoze jamii kuridhiana.

Amefafanua kuhusu maridhiano ilhali kuna viongozi wa kisiasa wanaoshikiliwa na vyombo vya dola, akisema kuridhiana hakupaswi kuchanganywa na uhalifu, kama mtu amevunja sheria anastahili kuwajibishwa kama raia mwingine.

Kauli hiyo ya Wasira inakuja wakati ambao, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amewahi kunukuliwa akihoji kama kuna haja ya maridhiano, ni nani na nani watakaoridhiana.

Alikwenda mbali zaidi na kuhoji chama hicho kinafikiriaje kuingia katika maridhiano, ilhali kiongozi wake (Mwenyekiti-Tundu Lissu), yupo mahabusu kwa kile alichokiita kesi za kisiasa.

Hoja ya haja ya maridhiano inaibuka kipindi hiki, kutokana na tukio la maandamano yaliyozaa vurugu yaliyotokea Oktoba 29 na 30, mwaka jana na kusababisha kuuawa kwa watu, uharibifu wa mali za umma na za watu binafsi.

Tangu kutokea kwa matukio hayo, kumekuwa na mvutano wa hoja, kati ya upande unaotaka maridhiano na ule unaoyapinga, ukisisitiza ili yafanyike lazima mambo kadhaa yatekelezwe na Serikali.

Wasira ametoa kauli hiyo katika mazungumzo yake, wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika ofisini kwake, Ofisi Ndogo ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Akilifafanua hilo, Wasira amesema maridhiano yanapaswa kuihusisha Serikali iongoze jamii kuridhiana, kwa kuwa kuna kundi kubwa lililoathiriwa.

“Jamii imeathirika sana na jamii ina watu wengi, ina vijana ambao wanasema ndio waliotoka kufanya (maandamano/vurugu), watu wazima walioathirika, jamii ina watu ambao ndugu zao wameuawa, waliopoteza mali wamechomewa nyumba.


“Hao wote ni jamii, sasa unapotaka kuridhiana lazima ulete makundi haya yote pamoja, tuzungumze jamani hapo ndipo tulipofika, tunatokaje, ndio tunaridhiana hapo sasa,” amesema.

Alipoulizwa maridhiano yatafanyikaje ikiwa kuna kesi za kisiasa, Wasira amesema hakuna kesi ya kisiasa nchini, isipokuwa watu wanakosea kudhani ukiwa na nafasi fulani una uhuru wa kutenda kosa halafu cheo kikulinde.

“Maridhiano sio badala ya sheria, maridhiano hayabadili sheria, hakuna aliye juu ya sheria, ukiwa kiongozi wa kisiasa unapaswa kuheshimu sheria, ukikosea utashtakiwa na kukamatwa kama raia mwingine,” amesema.

Amesema watu hawapaswi kuchanganya maridhiano na uhalifu, akidokeza kuna chama kimoja nchini mwanachama wao akikamatwa wanatangaza kukamatwa, bila kufafanua sababu.

Kwa namna chama hicho (hakukitaja) kinavyotangaza taarifa ya kukamatwa kwa mwanachama wake, amesema utadhani kosa ni kuwa mwanachama, kumbe mara nyingi kuna sababu nyingine.

Amesema Tanzania ina watu zaidi ya milioni 60 na sio kwamba wanaokosea ni wanachama wa chama fulani pekee, akisisitiza wapo wanachama wa CCM waliopo magerezani.

“Hakuna kesi za siasa, ukifanya makosa ukavunja sheria inakuwa kesi ya siasa? Kesi ya siasa huwa haiendi mahakamani, nenda nchi zote. Kesi ya kisiasa haikupi haki ya kujitetea,” amesema Wasira.

Matukio ya Oktoba 29 ni doa

Amekiri matukio hayo yameitia doa Tanzania, ingawa si mara ya kwanza kwani mwaka 1964, Jeshi la Tanganyika Rifles liliwahi kuasi, ikiwa ni miaka miwili baada ya kujitawala.

Kwa mtazamo wa Wasira, yaliyofanyika Oktoba 29, hayakuwa maandamano bali ni uasi, kwani yamefanyika usiku, hayakuendeshwa vema kama inavyopaswa.

“Wakaenda wakavunja ATM, halafu wakamaliza sijui walichukua hela kwa sababu kuna benki wanasema waliweka Sh80 milioni na hawakuzikuta, maandamano yalikula hela.


“Wametoka pale wameenda Igoma (Mwanza), wanaandamana kuingia benki usiku, sasa unayaitaje hayo maandamano. Hata shetani unaweza ukampa jina zuri tu kama ukimpenda sana, lakini huu ni uhalifu,” amesema.

Ameeleza ulifika wakati polisi walipiga risasi juu, lakini watu wakaendelea kuwafuata, ikalazimika wapige za moto kujihami, bado waliendelea.

Kuhusu tume ya kuchunguza yaliyotokea Oktoba 29

Ameeleza tume ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29, haikuundwa kuichunguza Serikali, bali kilichotokea, chanzo chake na mengine ni yatokanayo.

“Ukisema Serikali, kufa watu, mimi ni miongoni mwa watu wanaochukia sana watu kufa, mimi mwenyewe sipendi kufa, huwezi ukashangilia kufa watu,” amesema.

Lakini, amesema Serikali haikuingia mtaani na bunduki kutafuta na kuuwa watu, kulikuwa na sababu ambayo ni ghasia zilizotokea kutoka mahali kusikojulikana watu wakichoma majengo ya umma na mali za watu binafsi.

“Huwezi ukasema tume ile… mimi nawashangaa kweli, Jaji Chande (Othman, Mwenyekiti wa tume hiyo), amewahi kuaminiwa na Umoja wa Mataifa kuchukuza chanzo cha kifo cha Katibu Mkuu wa UN,” amesema Wasira.

Katika maelezo yake, amesema uwajibikaji hauwezi kuwa kwa Serikali pekee, bali utawahusisha walioratibu, akihoji vijana waliingiaje mitaani na kufanya uharibifu.

Kuhusu madai ya watu kulipwa, amesema si maelekezo kwa tume, bali ni maoni ya Serikali kwa kuwa linapotokea jambo muhimili huo kwa kawaida huwa na kitu unachokijua.

“Kama tume ikisema hazikuwepo fedha basi, lakini haya si maelekezo, hadidu za rejea ndio maelekezo. Nenda uchunguze ulete taarifa. Huwezi ukawa Rais halafu hujui kitu kabisa hadi tume ije,” amesema Wasira.

Mtazamo wake kuhusu haki, amani

Kwa mtazamo wa Wasira kuhusu mjadala wa nini kinatangulia kati ya haki na amani, amesema anakubaliana na wote, akisisitiza haki na amani ni kama kuku na mayai.

Alipoulizwa nini yai na nini kuku amejibu kwa kuhoji, “nani anaanza ni kuku anayetaga mayai au yai linalototoa kuku. Kwa sababu haiwezekani ukazungumza haki peke yake.”

Ameeleza panapokuwa na amani, hata ikikosekana haki inadaiwa kwa misingi ya amani, akisisitiza ni vigumu kutaka haki pasipo na amani.

“Kuna uhusiano mkubwa kati ya amani na haki, sawa na kuku na yai,” amesema Wasira.

Alipotakiwa kufafanua kuhusu taarifa ya kuchomwa kwa nyumba yake Bunda mkoani Mara, Wasira amesema asingependelea kueleza kwa kina kuhusu mambo binafsi na kungekuwa na watu ndani ingesikika wamefariki.


“Tuzungumze mambo ya nchi, mambo ya nyumba yangu, nitajenga nyingine na waliochoma na wao, Mungu yupo atataka kujua walichoma ili wapate nini,” amesema.

Hata hivyo, amesema haikuwa nyumba ya fahari na ameijenga kwa fedha zilizotokana na shughuli zake na kwa historia yake hakuwahi kuiibia Jamhuri ya Muungano, kwamba anao uwezo hata wa kuwasilisha taarifa za hesabu zake.

“Kwa historia yangu vitu nilivyonavyo nilikuwa napata posho nafanya ubunge na nikachukua posho za ubunge wa watu wa Bunda, nikajenga Bunda. Kwa kuwa wamechoma basi mimi ilimradi kazi yangu ya ubunge ilishafanyika, basi inabaki, hivyo hiyo sio hoja kubwa,” amesema Wasira.